Dar es Salaam. Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa Simba, Yanga na Azam huenda zikanogeshwa na mechi ambazo timu hizo tatu zitacheza katika viwanja na miji tofauti.
Wakati timu 16 kila moja ikishuka uwanjani leo kusaka pointi tatu dhidi ya nyingine, mechi tatu zitakazohusisha timu hizo tatu zinazowania ubingwa ndizo zinaonekana zitafuatiliwa kwa ukaribu.
Mechi hizo ni ile ya Simba itakayokuwa ugenini dhidi ya Lipuli ya Iringa, Azam itakayoikaribisha Coastal Union na Yanga itakayokuwa nyumbani kucheza na Prisons ya Mbeya.
Vinara Simba baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, itakuwa na kibarua kigumu Uwanja wa Samora huko Iringa dhidi ya timu isiyotabirika ya Lipuli.
Licha ya Simba kuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu hiyo ikipata ushindi mara mbili na kutoka nayo sare tatu tangu ilipopanda daraja misimu miwili iliyopita, vinara hao wa Ligi Kuu wanapaswa kuingia na tahadhari dhidi ya Lipuli. Timu hiyo inayoshika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 29 imekuwa na homa za vipindi na hilo linaweza kuigharimu Simba ikiwa itawadharau kwa kutazama mechi zao zilizopita ambazo hawakufanya vizuri.
Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili kali, Azam dhidi ya Coastal kwenye Uwanja wa Uhuru saa 10:00 jioni kabla ya Yanga kuikaribisha Prisons kwenye Uwanja wa Taifa saa 1.00 usiku.
Pia Soma
- Man City waijia juu Uefa kisa kufungiwa miaka miwili, kukata rufaa Cas
- Wachezaji watatu wa Simba kuikosa mechi na Lipuli
- Ronaldo afunga bao la utata Juventus
Timu hiyo inayonolewa na kocha Juma Mgunda, imepoteza mechi moja kati ya 11 za mwisho iliyocheza katika Ligi Kuu imeibuka na ushindi mara saba, kutoka sare mbili huku ikipoteza mchezo mmoja ambapo imefunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
Nidhamu ya wachezaji kufanyia kazi mbinu wanazopewa na Mgunda imeonekana kuwa silaha muhimu ambayo imekuwa ikiibeba Coastal katika mechi za hivi karibuni kulinganisha na mwanzoni.
Hata hivyo Azam imekuwa na kiwango bora na tangu ilivyofungwa na Coastal bao 1-0 mwishoni mwa mwaka jana, haijapoteza mchezo wa Ligi Kuu.
Kocha msaidizi wa Azam Iddi Cheche alisema wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo.
“Vijana wetu wako kambini lengo ni kujiweka vizuri na kuwa pamoja. Raundi ya pili imeanza na kila mmoja anataka kukusanya pointi ili atimize lengo lake,”alisema Cheche.
Baada ya mechi ya Azam, kivumbi kingine ni kile cha Yanga iliyotoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City itakayovaana na Prisons.
Ni mechi inayoonekana itakuwa ya upande mmoja zaidi ambao ni Yanga kwani Prisons haina kiwango bora katika siku za hivi karibuni. Maafande hao wanaingia uwanjani wakiwa wametoka kupoteza mechi ya mwisho dhidi ya Mbeya City.
“Tutamkosa Ditrama Nchimbi ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano. Haruna Niyonzima ni mgonjwa, Kelvin Yondani alipata majeraha katika mchezo uliopita, Feisal Salum pia ana majeraha,” alisema kocha wa Yanga Luc Eymael alipokuwa akizungumzia mchezo huo.