Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga, Azam ndani ya 2021

Simbasctanzania Vigogo wa Soka nchini walilia lakini pia walicheka

Tue, 7 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

2021 umekuwa mwaka wa vilio na vicheko kwa vigogo wa soka Tanzania Simba, Yanga na Azam FC kutokana na baadhi ya matukio yanayowahusu wao.

Ni mwezi mmoja pekee umesalia kufunga mwaka 2021, na kuuanza mwingine mpya 2022, Mwanaspoti linakuletea matukio mbalimbali yaliyozikumba timu hizo ndani ya mwaka huu 2021 na kukujuza namna ambavyo walilia na kucheka kupitia matukio hayo.

KUONDOKA LUIS, CHAMA

Hili ni pigo kubwa ambalo limewakuta Simba ndani ya msimu huu, kutokana na umuhimu wa nyota hao ndani ya kikosi cha kwanza msimu huu.

Licha ya Simba kuwa na kawaida ya kuwauza wachezaji wake, lakini kwa kuwauza nyota hao kumeonyesha pengo kubwa japokuwa waliwaongeza mastaa wengine kama Peter Banda, Sadio Kanoute, Duncan Nyon pamoja na Sakho.

LIGI YA MABINGWA

Simba ililia hapa baada ya matarajio yao ya kutinga hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa kushindwa kutimia baada ya kuondoshwa katika michuano hiyo na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-3.

Mchezo huo ulikuwa wa kusisimua Simba wakiwa na matumaini kibao baada ya kushinda ugenini mabao 2-0 na kwa Mkapa wakaanza kufunga lakini Jwaneng walipambana na kushinda mabao 3-1 na kufanya jumla ya mabao kuwa 3-3 yaliyowaondosha Simba kwenye michuano hiyo na kupelekea kumtimua kocha wao Mkuu Didier Gomes, lakini walipata kicheko baada ya kupelekwa kombe la Shirikisho.

Hata watani zao Yanga nao walilia baada ya kuondoshwa katika hatua ya awali ya michuano hiyo na Rivers United ya Nigeria na kujikuta wakiangukia pua baada ya kufungwa nyumbani na ugenini. Mchezo wa nyumbani Yanga ilikubali kichapo cha bao 1-0 matokeo hayo hayo sawa na ugenini na kujikuta wakiangukia pua.

FAINALI FA KIGOMA

Mchezo huu Simba alifurahi kama bingwa mtetezi huku Yanga aliyekuwa na matumaini kibao akilia kwa kupoteza mchezo huo.

Ilikuwa fainali ya aina yake ambayo Simba alikuwa anahitaji kupata matokeo baada ya kutoka kupoteza mchezo wa watani kwa kufungwa bao 1-0 hivyo nyota wake walipambana kuhakikisha wanapata matokeo na walifanikiwa.

KUSIMAMISHWA NYOTA AZAM

Uongozi wa Azam katika hili umeipelekea timu kulia kutokana na matokeo ambayo inayavuna baada ya kusimamishwa kwa nyota wake Mudathir Yahya, Agrey Morris pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Umuhimu wa nyota hao ndani ya kikosi cha kwanza cha Azam umepelekea timu hiyo kulia iwe ndani ya ligi na hata kombe la Shirikisho ikitolewa hatua ya awali.

YANGA USAJILI WA DJUMA/ MANYAMA

Djuma Shabani ni moja ya mastaa kutoka Congo katika klabu ya AS Vita aliyekuwa akitolewa macho na watani zao Simba kumnasa.

Yanga mabingwa wa kihistoria walipata kicheko baada ya kunasa saini yake huku Simba wakilia na kuamua kuachana nae baada ya kuzidiwa kete na wapinzani wao.

Huku Edward Manyama Azam FC iliwapiga na kitu kizito wapinzani wao Simba na Yanga ambao walikuwa mawindoni kunasa saini ya nyota huyo akitokea Ruvu Shooting inayonolewa na Kocha Charles Mkwasa.

Simba ndio ililia zaidi katika usajili huu licha ya Azam FC kumtangaza hata wao Simba walipigwa changa la macho na kumsajili nyota huyo wakimfuata yeye binafsi huku Azam wakiufuata uongozi wa Ruvu Shooting kutokana na kuwa na mkataba bado. Baada ya sintofahamu hizo, Yanga iliamua kujiweka kando na kuachana nae licha ya kuwepo kwenye rada zao.

UBINGWA NGAO YA JAMII

Yanga ilicheka vilivyo baada ya kuwapokonya Simba taji la kwanza katika mataji matatu ambayo walikuwa wanayashikilia la Ligi Kuu, FA pamoja na hilo na kuwafanya waanze vibaya msimu hasa mashabiki wao.

Ni Fiston Mayele aliyewalaza mashabiki wa Simba na jezi zao kutokana na matumaini waliyokuwa nayo kwa timu yao, huku wa Yanga wakitamba siku hiyo na nyota wao kujikuta wakioga noti.

UBINGWA LIGI KUU

Mwaka huu Simba ilicheka baada ya kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara ya nne mfululizo. Simba imetamba miaka minne mfululizo kulitwaa taji hilo hivyo ikiwaza na msimu huu itaweza kucheka au italia kutokana na kasi waliyonayo watani zao Yanga kwa sasa.

MAJERAHA YANAVYOWATESA

Simba imepata pigo baada ya nyota wao muhimu ndani ya kikosi cha kwanza Thadeo Lwanga na Chris Mugalu kuumia majeraha ambayo yatawaweka nje muda mrefu.

Mugalu anasumbuliwa na nyama za paja huku Lwanga aliumia goti majeraha ambayo yanawaweka nje ya dimba kwa muda mrefu sana. Hata Azam FC nao wamelia juu ya mshambuliaji wao mahiri Prince Dube ambaye aling’ara vilivyo msimu uliopita akiwania kitu cha dhahabu.

Lakini majeraha yalimuweka nje ya dimba kwa muda mrefu licha ya sasa kuanza mazoezi mepesi ya kuweka mwili sawa na kuanza kucheza. Yanga nao wamelia baada ya mshambuliaji wao Yacouba Sorgne kuumia goti na kufanyiwa upasuaji jeraha ambalo litamuweka nje ya dimba miezi mitano.

BASI LA AZAM

BASI aina ya Mercedes Irizar ambalo Azam FC imelinunua nchini Afrika Kusini na sasa inalitumia katika safari zake ndilo habari ya mjini katika medani ya soka nchini.

Thamani kubwa ya basi hilo pamoja na muundo wake wa kifahari lilizua gumzo kutokana na aina ya mapokezi ambayo ilikuwa ikiyapata katika maeneo mbalimbali iliyopita.

Wakati Azam wakicheka na basi lao, hata Simba ilipata mabasi matatu ya timu ya vijana, wanawake na timu kubwa kutoka kampuni ya Africarriers.

MO KUJIONDOA SIMBA

Ilikuwa kilio kwa mashabiki wa klabu hiyo, baada ya mwekezaji wao Mohamed Dewji ‘Mo’ kutangaza kujiondoa katika nafasi hiyo na kumpa kijiti Salim Abdallah ‘Try Again’. Kujiondoa huko kuliwaliza wanamsimbazi kutokana na namna ambavyo alikuwa akijitolea pesa zake ili timu hiyo iweze kufanya vizuri ikiwemo kuboresha bonas hasa katika michuano ya Kimataifa. Mbali ya kulia lakini walicheka baada ya mwekezaji huyo kuweka bil 20 katika akaunti zoezi lilokuwa likikwamishwa na tume ya ushindanio ya kibiashara (FCC) kuingilia kati mchakato wa uwekezaji.

MATAMASHA YALIVYOKUWA

Katika matamasha yao wote waliondoka na majonzi licha ya kuyaandaa wenyewe na kuzialika timu hizo kucheza nazo.

Yanga ilicheza na Zanaco katika mchezo wa kujipima nguvu kwenye kilele cha wiki ya wananchi na kujikuta ikiangukia pua baada ya kulizwa kwa kufungwa mabao 2-1.

Na watani zao Simba walitoka kinyonge Simba Day baada ya kufungwa bao 1-0 na TP Mazembe katika siku hiyo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz