Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Wasipobadilisha Haya, Itakula Kwao

Simba Waondoka Zam Simba Wasipobadilisha Haya, Itakula Kwao

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: Mwanaspoti

SIMBA imetinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika tangu kuanzishwa kwa mfumo huo 2009 baada ya kuiondoa Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-2.

Baada ya kutinga hatua hiyo huenda ikakutana na vigogo wa soka Afrika kutokana na rekodi walizonazo katika michuano hiyo au ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wawakilishi hao pekee wa nchi katika mashindano ya kimataifa walianza safari kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya mchujo na walitolewa na Jwaneng Galaxy.

Baada ya kuondolewa walidondokea Kombe la Shirikisho Afrika na kucheza hatua moja ya mtoano dhidi ya Red Arrows ambao licha ya kushinda nyumbani hawakusonga mbele kutokana na matokeo ya jumla. Mwanaspoti lilifuatilia kwa karibu mechi zote za Simba katika michuano hiyo - ile waliyocheza nyumbani na ugenini na kubaini kuna mambo wanalazimika kubadilika ili maisha yawe mazuri kwao katika michuano hiyo kufikia lengo la kucheza nusu fainali.

MABAO YA KROSI

Simba imeendelea kufungwa mabao mengi ya krosi kupitia kwa mabeki wa pembeni - Mohammed Hussein na Shomary Kapombe.

Baada ya krosi hizo kupigwa wamekuwa wakifungwa mabao ya vichwa kama ambavyo ilikuwa dhidi ya Jwaneng, Geita Gold, Ruvu Shooting na Red Arrows.

Mabeki wake wa kati na wachezaji wengine wamekuwa wakishindwa kuokoa mipira ya namna hiyo na kuwaacha wachezaji wa timu pinzani kuwa huru kupiga mpira wanavyotaka.

Katika mechi na Red Arrows zilipigwa krosi zaidi ya kumi, lakini ilitumika moja tu kufungwa bao ila nyingine zote walikosa wenyewe Arrows kwa wachezaji wa Simba kushindwa kuziokoa.

Kama Simba watakwenda na shida hii katika makundi kutokana na aina ya wapinzani wanaokutana nao watafungwa mabao mengi kama ilivyokuwa msimu wa 2018, kwenye mechi na Nkana Red Devils, JS Soura, AS Vita na Al Ahly.

WACHEZAJI KUCHOKA

Wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza Simba msimu huu wanaonekana kuchoka na kushindwa kutimiza majukumu kama ilivyokuwa misimu mitatu nyuma.

Miongoni mwa wachezaji hao ni nahodha John Bocco hayupo katika kiwango bora kama msimu uliopita aliomaliza akiwa mfungaji bora wa ligi na mabao 16 na kuwa mchezaji bora wa msimu.

Wachezaji wengine Hussein ‘Tshabalala’, Kapombe, Joash Onyango na Erasto Nyoni ni miongoni mwa ambao hawapo katika viwango bora na wanaonyesha kila dalili kuwa wametumika zaidi.

Pengine kuchoka huko kupunguza ubora wao ndio maana kocha wa Simba, Pablo Franco amekuwa akiwaweka benchi na kuwatumia wengine kama Israel Mwenda, Gadiel Michael na Henock Inonga.

UWANJA WA NYUMBANI

Kabla ya kupoteza dhidi ya Jwaneng katika mechi ya nyumbani, Simba walikuwa wakijiamini kuwa timu yoyote itakayokuja kwao kupata matokeo mazuri labda iwe sare.

Awamu hii mambo yamekuwa tofauti kwa Simba kushindwa kucheza kwa kujiamini nyumbani kama ilivyokuwa awali, jambo ambalo linawapa hali ya kujiamini wapinzani wao. Awali timu iliyokuja Benjamin Mkapa akilini iliamini kupata ushindi sio kazi rahisi na ilikuwa hivyo kwa Al Ahly, TP Mazembe, As Vita na nyingine nyingi.

Msimu huu baada ya kufungwa nyumbani mpinzani yeyote ambaye atakuja nchini kucheza na Simba anaweza kujiamini kupata matokeo mazuri.

Kwa hiyo akili za wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wanatakiwa kupambana kupata matokeo mazuri ugenini pamoja na nyumbani, huku wakiachana na rekodi za nyuma katika Uwanja wa Mkapa.

VIWANGO VYA WACHEZAJI

Tatizo lingine ambalo Simba limekuwa ndani ya kikosi chao msimu huu hasa katika mashindano ya kimataifa ni wachezaji kutokuwa katika viwango bora kwenye mechi mfululizo.

Ukimuangalia Bocco aliyecheza katika kiwango bora kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Jwaneng hajaonekana tena katika ubora ule.

Katika mechi hiyo Bocco alifunga mabao mawili ndani ya muda mfupi kipindi cha kwanza na tangu hapo hakuwahi kucheza katika ubora huo na huenda jambo hilo ndio linamfanya kuwekwa benchi.

Bernard Morrison aliyekuwa katika kiwango bora kwenye mechi ya kwanza na Red Arrows ukimuangalia ambavyo alicheza mchezo wa marudiano unaweza kusema sio yeye alikuwa chini mno.

Mashindano haya yanakutanisha wachezaji walio katika ubora na viwango imara kila mechi kama wakikutana na timu yenye wachezaji wa viwango vya kupanda na kushuka kama walivyoonyesha Simba msimu huu lazima watafungwa.

Mbali ya kurekebisha makosa wanatakiwa kuwa na mwendelezo wa viwango bora katika kila mechi iwe faida kwao kufanya vizuri, vinginevyo hawataweza kutoboa makundi.

WALIOSAJILIWA

Simba msimu huu imesajili wachezaji 12 ili kuongeza makali ya kikosi kuwa bora zaidi ya msimu uliopita, lakini mambo yamekuwa tofauti kwa wengi.

Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na kuonyesha ubora ni beki Mkongomani Inonga ambaye kila anayefuatilia soka nchini hahitaji maelezo mengi kuthibitisha kiwango chake.

Wengine wote waliosajiliwa hawana uhakika na viwango vyao licha ya baadhi kupata nafasi ya kucheza kama Sadio Kanoute na wengine kutocheza kabisa. Kutokana na viwango hivyo msimu huu wanatakiwa kuviboresha ili kwenda kushindana na wapinzani wao walio bora au kuingia sokoni kunasa wengine wenye viwango bora zaidi.

MBINU

Jambo lingine ambalo Simba limekuwa shida ni mabadiliko ya benchi la ufundi yamewafanya wachezaji kushindwa kunasa vyema mbinu za kocha mpya, Pablo Franco.

Kuna nyakati Pablo analazimika kutumia mifumo tofauti na ule wa 4-2-3-1, ila wachezaji wanashindwa kufanya vizuri katika aina nyingine ya uchezaji na kuamua kurudi hapo.

Wachezaji wanahitaji muda zaidi wa kukaa na kuelewa mbinu za kocha ambaye ameonyesha ni muumini wa kucheza soka la chini, kumiliki mpira muda mrefu na kushambulia kwa haraka. Kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakifiti katika mbinu ambazo anahitaji wacheze ila kuna wengine wamekuwa wakipitia wakati mgumu kutokana na viwango vyao kutakuwa bora.

MSIKIE BARBARA

Mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez anasema kikosi kimepambana na kufika hatua ya makundi, lakini lengo ni kucheza nusu fainali.

Barbara anasema kuna maeneo yamekuwa na shida katika kikosi na viongozi wamejipanga kuyafanyia kazi. “Tutasikiliza maoni na mapendekezo ya kocha Pablo ambayo atatukabidhi wiki ijayo kuna vitu gani vya msingi ambavyo anahitaji viongozi tumfanyie kazi,” anasema Barbara.

“Kutokana na kikosi ambavyo tumekiona kwenye dirisha dogo lazima tutakwenda kufanya maamuzi magumu hasa katika suala hili la usajili.”

Chanzo: Mwanaspoti