Uongozi wa Simba, umeweka wazi kuwa, kuelekea mchezo wao dhidi ya Raja Casablanca, wapo tayari na wameanza maandalizi ili kupata matokeo chanya.
Juzi Ijumaa, Simba ilianza maandalizi kwa ajili ya mchezo huo wa mwisho Kundi C katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni siku sita wanatarajia kuzitumia kufanya mazoezi kabla ya kukwea pipa kuwafuata Raja Casablanca kwenye mchezo wa mwisho unaotarajiwa kuchezwa Aprili Mosi, mwaka huu nchini Morocco.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema, kikosi chao kinatarajiwa kuelekea Morocco Machi 30.
“Maandalizi yapo sawa, baada ya kumalizana na Horoya wachezaji walipata muda wa kupumzika, kisha wakaanza mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Raja Casablanca.
“Utakuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa ukizingatia tutakuwa ugenini, lakini ambacho tunahitaji ni kufanya vizuri ugenini kwani inawezekana,” alisema Ally.
Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufikisha pointi 9 katika Kundi C ambazo haziwezi kufikiwa na Horoya na Vipers, zote zikisaliwa na mechi moja. Vinara ni Raja wenye pointi 13.