- katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi.
Simba ilikubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Kaizer Chiefs kwenye mechi hiyo ya robo fainali ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa FNB nchini humo Jumamosi iliyopita, hivyo inahitaji ushindi kuanzia mabao 5-0 ili kutinga nusu fainali.
Lakini Mratibu wa klabu hiyo, Abbas Ally, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwataka kuendelea kuisapoti timu wakati wote kwa kuwa kama wao waliweza kuwafunga kwao hata Simba inaweza kushinda nyumbani.
"Mpira mara nyingine una matokeo ya kikatili, lakini tunawaomba mashabiki wetu ambao wamekuwa wakitusapoti muda wote bila kujali matokeo waendelee kutusapoti, tutaishangaza dunia kwa kile ambacho tutakwenda kukifanya hapa.
"Tunaenda kuanza maandalizi, kama wao waliweza kutufunga kwao na sisi tunaweza kuwafunga kwetu. Kama CAF (Shirikisho la Soka barani Afrika), itatupa nafasi ya mashabiki kuingia uwanjani, waje kwa wingi Jumamosi kutusapoti.
"Tunapofungwa na kushinda wamekuwa pamoja nasi, kile walichokifanya wazee wetu miaka ya 75 tunakwenda kukirudia," alisema.
 Abbas alisema Simba si timu ya kwanza kufungwa mabao manne na kufafanua kuwa hata Brazil iliwahi kukutana na kipigo kikali cha mabao saba kwenye Kombe la Dunia, hivyo Simba kufungwa si kitu cha ajabu.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema: "Hatuna majeruhi yeyote, tumewapa wachezaji mapumziko ya siku moja na kesho [leo] jioni wataingia kambini kuanza maandalizi ya mechi ya marudiano, kesho [leo], tunazunguza zaidi na waandishi wa habari."
Kwa upande wa Kocha Mkuu, Mfaransa Didier Gomes, tayari alishaeleza: "Jambo lolote linawezekana kwenye mpira, hatujafurahia matokeo lakini bado tuna matumaini, ni muhimu sana kuamini kwamba tunaweza kubadili matokeo. Lakini kama tunataka kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa marudiano lazima tuwe bora zaidi."
Wakati huo huo, winga wa timu hiyo, Mghana Bernard Morrison, ambaye hakusafiri na timu yeye ametuma ujumbe kupitia mtandao wake wa Twitter akieleza: "Wakati shujaa anapojikwaa, waoga hufurahi. Hakuna anayehisi vizuri kwa mwoga kuliko kuona mtu mzuri akianguka. Wakati wanasema huwezi kufanya, waambie wakae chini na kuangalie jinsi unavyofanya."
Katika michuano hiyo hatua ya awali mwaka 1979, Simba ilikubali kipigo cha mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Mufulira Wanderers FC ya Zambia na ilipokwenda ugenini ikapindua 'meza' kwa kushinda 5-0 na kusonga mbele.