Wakiwa wanajiandaa kuivaa na Power Dynamos katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, uongozi wa Simba SC umetangaza kuja na hesabu mpya kwenye michuano hiyo msimu huu kwa kuweka wazi malengo yao ni kuandika rekodi ya kucheza Nusu Fainali ya mashindano hayo.
Simba SC ambao wanaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, wanatarajiwa kushuka Uwanja wa Levy Mwanawasa nchini Zambia kuvaana na Power Dynamos, mchezo utakaopigwa Septemba 16, mwaka huu.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Simba SC katika mashindano hayo msimu huu, ikiwa imepangwa kuanzia hatua ya kwanza kwa kanuni za ubora wa viwango vya CAF, huku wakiwa na kumbukumbu ya kuishia Robo Fainali ya mashindano hayo msimu uliopita.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema: “Hamasa na maandalizi ya mchezo huu ni makubwa, tayari tumefanikiwa kukusanya kundi kubwa la mashabiki ambao tutasafiri nao.
“Huu ni mchezo ambao unaenda kutupa uelekeo wa hesabu zetu za msimu ambapo kama timu tumeweka malengo ya kucheza angalau hatua ya Nusu Fainali ya mashindano haya hasa kwa kuwa tumekuwa na historia ya kumaliza Robo Fainali kwa misimu kadhaa sasa, hivyo msimu huu tunaitaka rekodi ya tofauti.”