Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba: Sisi ni ubingwa tu

Ndoo Pic Data Simba wanacheza leo dhidi ya Polisi Tanzania

Sun, 10 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba tayari ipo mjini Moshi kwa ajili ya pambano lao la leo la Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania ikiwa ni saa chache tangu itoke kuifumua Coastal Union kwa mabao 2-1, huku akili zao zikiwa kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabosi wa timu hiyo akiwamo Kocha Pablo Franco wamesisitiza wanataka kutimiza malengo yao, lakini kuwa ni kuhakikisha wanafika fainali ya Afrika na kubeba ubingwa, huku wakipambana kuitetea mataji yao ya Ligi Kuu na Kombe la ASFC.

Ushindi wa juzi dhidi ya Wagosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, umerejesha matumaini makubwa kwa Pablo katika kutetea ubingwa wa Bara, lakini akisema akili zake kwa sasa zipo kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Pablo alisema malengo yao makubwa msimu huu ni kufika mbali kimataifa hivyo anazingatia hilo kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji ili kuhakikisha hawapati majeraha mara kwa mara.

“Tupo kwenye michuano mitatu na yote lengo letu ni kufika mbali na kutwaa mataji hivyo lazima tuhakikishe tunalinda afya za wachezaji wote kwenye kila mchezo.

“Tutaendelea kufanya mabadiliko na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine ili kila mmoja awe timamu katika kitimiza majukumu yake na malengo ya timu,” alisema.

Juu ya mechi yao ya kesho alisema: “Polisi ni timu nzuri, lakini tunachohitaji ni ushindi jambo ambalo linawezekana kwani kila mchezaji anajua umuhimu na uhitaji wa pointi tatu kwenye mechi hiyo.

“Baada ya hapo tutaingia kambi maalumu ambayo kila kitu kitakuwa kuhusu mchezo dhidi ya Pirates ambao ni lazima tushinde nyumbani ili kutengeneza mazingira ya kufuzu.

“Tunajua Pirates ni timu bora na ngumu, lakini hadi kufika hatua hii basi kila timu ina ubora wake. Hata wao wanalifahamu hilo hivyo tunatarajia kuwa na mchezo mzuri, na imani tukifanya vizuri tutakuwa na nafasi ya kufika fainali na hata kuchukua ubingwa. Hakuna kisichowezekana.”

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya wa Simba, Mwina Kaduguda alisema kuwa wapo tayari kufa ila Simba ifanikiwe na kufikia malengo yao kwa msimu huu.

“Tunaziona timu zilizofanikiwa Afrika kuwa na uwekezaji mkubwa. Simba pia tupo kwenye njia hiyo kwa msimu wa tano sasa kwanini tusifanikiwe kubeba mataji makubwa Afrika?” alihoji katibu mkuu na kaimu mwenyekiti huyo wa zamani wa Simba na kuongeza:

“Tunaamini tunaweza kumfunga yeyote na kutwaa mataji kama ilivyo lengo letu na nipo tayari kufa ili kuhakikisha Simba inafikia malengo na kutwa mataji makubwa makubwa Afrika.”

Simba inahitaji kuiondosha Pirates katika Kombe la Shirikisho ili kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kupitia mechi mbili ambapo Aprili 17 itaanzia nyumbani kisha mechi ya marudiano itakuwa ugenini Aprili 24 mwaka huu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz