Wakati joto la pambano la watani wa jadi Simba na Yanga likianza kupanda wenyeji wa mchezo huo Simba imetoa kauli nzito ikisema hawako tayari kuwaona wapinzani wao wanatangaza ubingwa mbele yao.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja mawasiliano wa Simba Ahmed Ally akisema kuelekea mchezo wa Aprili 16 klabu yao haitakuwa tayari kugeuzwa ngazi ya Yanga kuufuata ubingwa.
Ahmed amesema hata kama Simba itakosa ubingwa lakini wamewaambia wachezaji wao kuwa jambo la Yanga kushinda mbele yao wakati wakielekea kuchukua ubingwa halikubaliki.
"Hii historia mbaya tukiiruhusu itaishi vizazi na vizazi, Simba haiwezi kukubali hili litokee, tutakuwa na dakika tisini za kwenda kulinda heshima ya Simba mbele ya watani wetu.
"Tumewaambia wachezaji wetu kwamba huu ni mchezo mkubwa kuliko yote na matokeo yake yatatupa heshima au kutubomoa lakini kubwa hatutakubali kugeuzwa ngazi ya ubingwa na Yanga.
“Tunaweza kudondoka tukaukosa ubingwa wa Ligi, lakini hatutaki kumpa mtu nafasi ya kutangazia ubingwa kwenye mgongo wetu. Lazima atambue kuwa hii ni Simba Sc.
“Katika mara zote ambazo Yanga anatufunga au kupata sare, huwa anabahatisha. Hawajawahi kuwa na ubora wala ‘standard’ ambayo Simba tunayo," amesema Ahmed ambaye klabu yao ipo nafasi ya pili kwenye msimamo.
Yanga ambao ndio vinara wa msimamo wa ligi wanakutana na Simba huku mabingwa hao watetezi wa ligi endapo watashinda mchezo huo wa Jumapili itahitaji ushindi wa mchezo mmoja pekee kuwa mabingwa.