Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba SC yapeleka 'mashushushu' Libya

Fadlu Na Simba Simba SC yapeleka 'mashushushu' Libya

Fri, 23 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Simba tayari wameanza mikakati ya kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kutuma 'mashushushu' nchini Libya ili kujipanga kuelekea mechi yao ya hatua ya kwanza ya michuano hiyo.

Timu hiyo ya jiji la Tripoli inatarajia kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Uhamiaji kusaka tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Benchi la ufundi la timu hiyo ambalo liko chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kwa kushirikiana na uongozi wao, wametuma ujumbe maalum ili kuishuhudia Al Ahaly Tripoli ambao huenda wakakutana katika mechi ya hatua ya kwanza ya michuano hiyo.

Ikumbukwe mchezo wa kwanza, Al Ahaly Tripoli iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uhamiaji na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo ambapo itakutana na Simba.

Taarifa zilizopatikana jijini zinasema Simba imetuma ujumbe wa watu wawili nchini Libya ili 'kuipeleleza' timu hiyo na kuandaa mikakati ya kuwakabili watakapokutana.

Chanzo hicho kilisema uamuzi wa kuwafuata wapinzani wao umefanya na Fadlu ili kupata taarifa sahihi za wapinzani wao.

"Inaonekana Waarabu hao wa Libya wana nafasi kubwa ya kusonga mbele na kukutana na sisi, benchi la ufundi limetaka kupata taarifa za kina za timu hiyo, ndio sababu ya kutuma wataalamu kwenda kuiangalia na baadaye kutoa ripoti kwa kocha, wana nafasi kubwa ya kukutana na sisi hatua inayofuata," chanzo hicho kilisema.

Yanga, Azam FC zinazoshiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika zimeanzia hatua ya awali sawa na Coastal Union ambayo inachuana kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa sasa Simba inaendelea na maandalizi ya mechi yake ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Fountain Gate FC itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wekundu hao wa Msimbazi walianza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi wa mabao 3-0, wakiifunga Tabora United kutoka mkoani Tabora, shukrani kwa Che Malone, Valentino Mashaka na Awesu Awesu kwa kupachika mabao hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live