Kampuni ya SportPesa imewakabidhi Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Shilingi Milioni 50 kama zawadi ya klabu hiyo kufika Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC iliishia Robo Fainali kwenye michuano hiyo, baada ya kuondoshwa kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati 4-3 na Orlando Pirates ya Afrika Kusini mwezi April.
Timu hizo zilipigiana Mikwaju ya Penati baada ya kutoka sare ya 1-1, huku kila timu ikishinda katika uwanja wake wa nyumbani 1-0.
Leo Jumanne (Mei 10), Afisa Metndaji Mkuu wa Simba SC Barbara Genzalez ameuwakilisha Uongozi wa klabu hiyo kupokea mfano wa hundi ya Shilingi Milioni 50, kutoka kwa Mkurugenzi wa SportPesa Tanzania Tarimba Abbas , katika hafla maalum iliyofanyika Jijini Dar es salaam.
Simba SC kupitia kurasa zao wa mitandao ya Kijamii imethibitisha tukio hilo kufanyika kwa kuandika ujumbe: “Mdhamini mkuu, kampuni ya SportPesa imetukabidhi Tsh. 50 milioni kama zawadi ya kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. #NguvuMoja”
Simba SC ilianza safari ya ushiriki wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa barani humo kwa faida ya bao la ugenini na Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Simba SC ilicheza dhidi ya Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa mtoano na kupata ushindi wa 3-0 ikiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na ilipoteza ugenini mjini Lusaka kwa kufungwa 2-1.
Ikiwa hatua ya Makundi Simba SC ilimaliza nafasi ya pili kwa kufikisha alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikibaki na alama 09 na US Gendamarie ya Niger iliburuza mkia kwa kuwa na alama 05.
Katika hatua ya Makundi Simba SC ilishinda michezo mitatu nyumbani jijini Dar es salaam na kutoka sare mchezo mmoja ugenini dhidi ya US Gendamarie, huku ikipoteza michezo miwili dhidi ya RS Berkane na ASEC Mimosas ugenini.