Wachezaji wa Simba SC wameahidi kucheza kwa nguvu ili kuhakikisha wanapata ushindi katika Mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca utakayochezwa keshokutwa Jumamosi (Desemba 09) jijini Marrakech, Morocco.
Kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kiliwasili salama jana Jumatano (Desemba 06) kikiwa chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha na kuanza mazoezi kuelekea mchezo huo wa tatu wa hatua ya makundi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mara baada ya kutua Marrakech, Benchikha alihitaji kuanza mara moja mazoezi ili kuhakikisha nyota wake wanaimarika na kuwa tayari kwa mapambano.
“Kocha alihitaji siku tatu za mazoezi, siku ya Jumatano, Alhamisi (leo) tutaendelea na Ijumaa pia, kabla ya kucheza mechi yetu Jumamosi kwa ajili ya kupigania kuondoka na pointi tatu dhidi ya Wydad na hii yote amezingatia zaidi katika utimamu wa mwili.
Amesema (kocha), kikosi chetu kiufundi kikosi vizuri, lakini tatizo ni utimamu na kwa sababu hiyo ameomba siku hizo ili kukiweka sawa,” alisema Ahmed.
Nahodha msaidizi wa Simba SC, Mohamed Hussein Zimbwe Jr, amesema wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo na wanatarajia kusaka ushindi wa ugenini licha ya kufahamu wanakutana na timu kubwa.
“Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, ila najua utakuwa mchezo mgumu kwa sababu wenzetu hawajapata matokeo yoyote ya ushindi mpaka sasa lakini sisi tuna pointi mbili katika kundi, tunafahamu ugumu wa Wydad, ugumu wa kundi letu, lakini tunafahamu umuhimu wa kuzipata pointi tatu,” amesema beki huyo wa kushoto.
Neye Winga wa timu hiyo, Jose Luis Miquissone, amesema kikosi chao kipo kamili kwa ajili ya kupambana ili kuwarudishia furaha wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
“Nafikiri tupo tayari kwa mechi hiyo, tutapigana, tupo tayari kwa mapambano, najua ni ngumu, Wydad ni timu kubwa na nzuri, lakini tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kwa ajili ya wanachama na mashabiki wetu na nchi kwa ujumla, watusapoti, tutawafanya wawe na furaha na hii ndiyo nafasi ambayo endapo tukishinda tutajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye kundi letu,” amesema nyota huyo raia wa Msumbiji.
Simba inashika nafasi ya tatu katika Kundi B ikiwa na pointi mbili wakati Wydad Casablanca ambayo haina pointi hata moja.