Kocha Msaidizi Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema kikosi chao kinakwenda kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC.
Simba SC itakua mwenyeji katika mchezo huo utakaopigwa Januari 17 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na uchungu wa kuutema ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Baada ya kuwasili jijini humo leo Ijumaa (Januari 06) majira ya Mchana akitokea Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’ sambamba na kikosi, Kocha Mgunda amesema, maandalizi ya kuikabili Mbeya City yanaanza mara moja, kwa kushirikiana na Bosi wake Robertinho.
“Tumerudi na kikubwa ni kwamba Kocha Mkuu mmemuona, kwa hiyo tunakwenda kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.”
“Kuhusu maandalizi ya mchezo wetu na Mbeya City, ninaamini ukifika muda tutazungumza, kwa hiyo kwa sasa mtuache ili tukafanye kazi.” amesema Mgunda
Mara ya mwisho Simba SC ilishinda mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuichapa Tanzania Prisons mabao 7-1, huku ikifikisha alama 44 nyuma ya Young Africans inayoongoza Msimamo kwa kuwa na alama 50.
Mchezo wa Duru la Kwanza dhidi ya Mbeya City FC, Simba SC ililazimishwa sare ya 1-1 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.