Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa wala hauna haja ya kupiga makelele mengi juu ya timu yao na wanachokifanya ni kuendelea kushinda mechi zao bila makelele na mwisho wa siku watu watashangaa kuhusiana na mafanikio yao ya msimu huu.
Simba kwenye ligi kuu msimu huu wanakamata nafasi ya pili wakiwa wameshinda michezo yote mitatu wakiwa na jumla ya pointi 9 huku kwenye Ligi ya Mabingwa wakihitaji ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos ili kutinga hatua ya makundi.
Akizungumza nasi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally alisema kuwa: “Simba wala hatuhitaji makelele mengi na badala yake tutafanya mambo yetu kimyakimya kuhakikisha kuwa tunatimiza malengo yetu.
“Hatutaki kusikiliza makelele ya wengi na tunachokihitaji kutoka kwa wachezaji wetu ni kuona katika kila mechi basi tunapata ushindi na wala sio jambo lingine kwani ubingwa haupatikani kwa mpira mzuri bali matokeo ya ushindi.
“Kwenye michuano ya kimataifa tunahakikisha kuwa kwanza tunapata matokeo mazuri, ili tusiweze kuishia njiani kwani Simba ni aibu kuona tunaishia hatua kama hii na ili kufikia malengo lazima tufikie tulipoishia ambapo ni robo fainali na kutafuta hatua kubwa zaidi ya hapo.”