Leo Septemba 2, 2022 wadhamini rasmi kwenye maswala ya usafiri wa klabu ya Simba ambao ni Africarriers wamekabidhi basi jipya ambalo litakuwa likitumiwa na kikosi cha timu ya wanawake cha Simba Queens na kufanya timu hiyo kuwa timu ya kwanza kwenye soka la wanawake kumiliki basi rasmi kwa safari zao mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari Mtengaji Mkuu wa klabu ya simba Barbara Gonzalez ameweka wazi kuwa mafanikio hayo waliyoyapata yametokana na kufanya vizuri kwa timu hiyo.
Kwa sasa imefuzu kushiriki ligi ya mabingwa Afrika kwa upande wa wanawake na kutanabahisha kuwa kwasasa wapo katika mchakato wa kutafuta mdhamini mkuu wa Simba Queens na tayari wapo kwenye mazungumzo na wadhamini wao hao wa Africarriers kwenye hilo.
Akijibu maswali ya wanahabari wakati wa makabidhiano ya basi hilo, Mtendaji Mkuu huyo wa Simba ametoa ushauri kwa klabu nyengine kwenye soka la wanawake nchini na kusema:
“Kwanza ni uwekezaji kwenye usajili, pili ni kutafuta namna nzuri ya kukuza jina la taasisi na tatu ni mahusiano mazuri na taasisi nyingine mbalimbali, lakini cha muhimu zaidi ni usajili mzuri ndio utakaoleta hayo mengine yote”.