KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema kikosi chake kiko vizuri na kila mechi kwao ni sawa na fainali sababu wanahitaji kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili jijini, Dar es Salaam jana, Mgosi alisema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa Juni 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani humo.
Mgosi alisema wamejipanga kuondoka na ushindi katika michezo mitatu ya kwanza ili kutangaza ubingwa wa ligi hiyo mapema msimu huu.
Kiungo huyo wa zamani wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, alisema kikosi chake kinatarajia kuondoka jijini Ijumaa kuelekea Ruvuma kwa ajili ya kukabiliana na wenyeji wao.
"Tumerejea na upepo wa kisulisuli, hatuachi mtu salama, kikosi kipo imara malengo yetu ni kushinda michezo mitatu ikiwamo dhidi ya Ruvuma Queens, Yanga Princess na JKT Queens, nina uhakika wa kutwaa taji hilo," alisema Mgosi.
Alisema wanawaheshimu Ruvuma Ila wamejipanga kuhakikisha wanapata alama muhimu katika michezo hiyo ili kufikia malengo yao ya kutwaa taji la ubingwa msimu huu.
JKT Queens ndio mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo wakifuatiwa na Simba Queens wakati Alliance Queens iko katika nafasi ya tatu.