Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Queens yafanya mauaji ya kutisha Tabora

91ffc9e552b39e7c81ec8129c77e8c26 Simba Queens yafanya mauaji ya kutisha Tabora

Wed, 13 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SIMBA Queens juzi ilifanya mauaji baada ya kuifunga ES Unyanyembe kwa mabao 16-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.

Licha ya ushindi huo, Simba imeendelea kubaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo saba, huku timu nyingine zikiwa zimecheza michezo nane.

Katika mchezo huo mabao sita yalifunga na Oppah Clement, Shelda Boniphace aliweka kimiani mabao matano, Mwanahamisi Omar alipiga hat trick na Omita Bertha alifunga mawili.

Katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Yanga Princess iliifunga Mapinduzi Queens kwa mabao 7-0 na kuendelea kusalia kileleni ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza michezo nane.

Mabao hayo yaliwekwa kimiana na Grace Yusuph, Aisha Masaka, Amina Ally ambao walifunga mabao mawili kila mmoja na Aniela Uwimana aliyefunga bao moja.

JKT Queens ikicheza katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam iliifunga Ruvuma Queens kwa mabao 2-1, ambapo mabao ya JKT yalifungwa na Zabela John na Mwamvua Seif na lile la Ruvuma lilifungwa na Amina Ramadhan.

Kwa matokeo hayo, JKT imefikisha pointi 21 katika nafasi ya pili baada ya kucheza michezo nane.

Alliance Girls ikicheza nyumbani iliifunga Tanzanite Queens kwa mabao 3-2 na kufikisha pointi 19 katika nafasi ya tatu na mabao mawili ya Alliance yalifungwa na Aisha Juma na Aliya Fikiri na ya Tanzanite yote yalifungwa na Asnath Linus.

Timu ya Baobab Queens ikicheza ugenini katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza iliifunga TSC kwa mabao 6-1 na kuendelea kusalia katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 13, mabao ya Baobab manne yalifungwa na Jamila Rajabu, Martha John na Rehema John walifunga bao kila mmoja na lile la TSC lilifungwa na Khadija Petro.

Nayo Mlandizi Queens ikicheza ugenini Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, iliifunga Kigoma Sisterz kwa mabao 3-0 na kufikisha pointi 11 katika nafasi ya sita, na mabao mawili yalifungwa na Shehat Juma na Rehema Ramadhan.

Chanzo: habarileo.co.tz