Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Queens waanza na kichapo Ligi Kuu Wanawake

Simba Queens Waanza Simba Queens waanza na kichapo Ligi Kuu Wanawake

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ya Wanawake, Simba Queens wameanza vibaya msimu huu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa JKT Queens.

Jkt Queens ni kama wamevunja mwiko kwani wamekuwa timu ya kwanza kuifunga Simba Queens kwenye uwanja wa Mo Simba Arena, kwani wekundu hao wa Msimbazi hawakuwahi kupoteza mchezo dhidi ya timu yoyote tangu waanze kucheza ligi kwenye uwanja huo mwaka 2020.

Fatuma Mustapha, "Kitunini' ndio amepeleka kilio Msimbazi baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 45 katika mchezo huo uliofanyika leo Desemba 6 kwenye uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.

Bao hilo ni la kwanza kwa Kitunini msimu huu tangu arejee kutoka katika majeraha ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja kwa mwaka mmoja na nusu huku bao lingine likifungwa na Etoo Mlenzi dakika ya 32.

Kitunini mmoja wa mastraika hatari nchini na tegemeo kwa JKT Queens aliumia mwanzoni mwa mzunguko wa kwanza katika msimu wa 2020/2021 akiwa amepachika wavuni mabao 20, msimu ambao Aisha Masaka wa Yanga aliibuka mfungaji bora akiwa amefunga mabao 35 akifuatiwa na Opah Clement wa Simba aliyefunga mabao 34.

Msimu uliopita Kitunini hakucheza kabisa na amerejea msimu huu kwankufunga bao lake la kwanza huku akitamba kuendeleza moto wa ufungaji.

Katika mchezo wa leo Simba Queens ndio walianza kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa Opah Clement aliyefunga kwa penalti baada ya winga Pambani Kuzoya kuangusha ndani ya eneo la hatari.

Opah ameendeleza rekodi yake ya msimu miwili mfululizo ya kufunga bao katika mechi ya kwanza ya ligi kwani msimu wa 2020/2021 alifunga mabao mawili walipoichapa Mapinduzi Queens mabao 4-2 na pia alifunga hat-trick katika mechi ya kwanza walipoibamiza Ruvuma Queens mabao 15-0.

Ni kama Simba ilikiwa haina bahati leo kwani dakika ya 79 baada ya kiungo Vivian Corazone kukosa penalti aliyopiga shuti lililopaa juu ya lango.

JKT Queens ilikuwa bora sana eneo la kiungo ikiongozwa na nahodha, Donisia Minja ambaye aliwapoteza viungo wa Simba walioongozwa na Corazone na Joelle Bukuru na kuwafanya maqueens hao wa Msimbazi kushindwa kucheza kwa kiwango bora.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live