Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Queens mzigoni, maajabu mengine yaja

Simba Queens Qq Simba Queens mzigoni, maajabu mengine yaja

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Simba Queens leo saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania itacheza mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake dhidi ya bingwa mtetezi wa michuano hiyo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa Simba kushiriki michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya pili, imefikia lengo ambalo ililikuwa ni nusu fainali na sasa inauwaza ubingwa. Simba ndio wawakilishi pekee wa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kwenye michuano hiyo na iliungana na timu nyingine saba kutoka kanda nyingine kutimiza timu nane zilizoshiriki fainali hizo zinazoendelea Morocco.

Simba ilipangwa kundi A na timu za Determine Girls ya Liberia, Green Buffaloes ya Zambia na wenyeji AS FAR ya Morocco na kucheza mechi tatu ikianza kwa kupoteza kwa mabao 2-1 mbele ya AS FA, na kushinda 2-0 dhidi ya Buffaloes na 2-0 Determine.

Matokeo hayo yamefanya Simba kushika nafasi ya pili kwenye kundi hilo na alama sita na kuungana na AS FAR iliyoongoza na alama tisa kutinga nusu fainali. Kutinga nusu fainali Simba imevuna Dola 200,000 (Sh 466 milioni) ambazo ni zawadi ya kufika hatua hiyo.

MPINZANI YUKOJE

Mamelodi ilikuwa kundi B na Bayelsa ya Niger, TP Mazembe na Wadi Degla ya Misri na kushinda mechi zote tatu ikiongoza kundi na kutinga nusu fainali na Bayelsa. Katika mechi hizo, Mamelodi iliichapa Bayelsa mabao 2-1, ikaifunga mabao 5-0 Wadi Degla na kuipiga TP Mazembe mabao 4-0 ikaongoza kundi jambo lililoifanya kukutana na Simba iliyoshika nafasi ya pili kundi A.

Kocha mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula anasema wanatamani kutinga fainali na kuchukua ubingwa.

“Kila timu huku imejipanga vizuri, tutacheza na Mamelodi moja ya timu imara na zenye uzoefu wa kutosha lakini tunaendelea kujipanga ili tufanye vizuri na kutinga fainali,” anasema Lukula.

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kushiriki mashindano hayo ikiwa ni msimu wake wa pili kufanyika huku Mamelodi ikishiriki kwa mara ya pili baada ya kuchukua ubingwa mwaka jana nchini Misri. Sambamba na mechi ya Simba na Mamelodi saa 4:00 usiku kutapigwa nusu fainali ya pili kati ya AS FAR na Bayelsa na washindi wa mechi hizo watatinga fainali huku zitakazopoteza zitapambania nafasi ya tatu.

Hiyo ni kwa mara ya pili mashindano hayo kufanyika, na msimu wa kwanza ilikuwa 2021 yalipofanyika Misri na Mamelodi kutwaa ubingwa kibabe kwa kuichapa 2-0 Hassan Ladies ya Ghana kwenye fainali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ anasema kinachofanyika sasa ni faida za uwekezaji waliouweka kwenye timu hiyo.

“Tulikuwa na malengo ya kufikia hatua ya nusu fainali.Haikuwa rahisi tulipigana hatimaye tumefikia hapo. Bado tunapambana kuhakikisha tunajenga heshima na kuandika historia kwa kuwa msimu wa kwanza kufanya vyema,” anasema.

Kocha msaidizi wa Fountain Gate Princess, Juma Masoud anasema: “Sina wasiwasi na ubora wa timu zote mbili kwa sababu wote wana vikosi vizuri.”

Chanzo: Mwanaspoti