Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake umemalizika huku Mabingwa wa Soka Tanzania, Simba Queens, wakiwa kileleni mwa msimamo.
Mechi ya mwisho ya mzunguko huo ilikuwa juzi wakati Baobab ilipotoka suluhu dhidi ya Alliance Girls kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Simba Queens sasa iko kileleni ikiwa na pointi 22 kwa michezo tisa ambayo imecheza, ikishinda mechi saba, sare moja, ikipoteza moja, ikipachika mabao 29 nyavuni na kuwa timu inayoongoza kwa kuwa na mabao mengi mpaka sasa.
Haikuwa rahisi kwa timu hiyo kufika hapo, kwani ilibidi isubiri hadi raundi ya sita ndipo ilipofanikiwa, huku raundi zote hizo zilikuwa zikiongozwa kwa maafande wa JKT Queens ambayo msimu huu imeonekana inauhitaji ubingwa kwa udi na uvumba.
Ni timu ambayo inaonekana kuwa mshindani mkubwa wa Simba Queens kwenye kulisaka taji hilo.
JKT Queens kwa sasa imeshushwa hadi nafasi ya pili, lakini imeendelea kung'ang'ania hapo hapo hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ikiachwa pointi moja tu na Simba Queens.
Ina pointi 21 ikicheza mechi tisa, kushinda sita, sare tatu na ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, ikifunga mabao 23.
Timu ya Fountain Gate Princess, imemaliza mzunguko huo ikiwa kwenye nafasi ya tatu ikijikusanyia pointi 20, huku Yanga Princess ikiwa kwenye nafasi ya nne na pointi hizo hizo 20.
Timu hizo zinafanana kwa mechi zilizocheza, zote zilishinda mechi sita, sare mbili na kupoteza moja kila moja, zikifunga mabao 21. Hata hivyo, Fountain Gate Princess imefunga mabao manne ambayo ni machache dhidi ya Yanga ambayo imeruhusu mabao matano na kuifanya kuwa chini yake.
Nafasi ya tano inashikiliwa na Alliance Girls ikiwa na pointi 15 na timu inayoshika mkia ni Mkwawa Queens yenye pointi moja mpaka sasa.
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unatarajiwa kuanza tena Aprili 18, mwaka huu, Baobab itakapocheza dhidi ya Fountain Gate Princess Uwanja wa Jamahuri Dodoma, The Tigers Queens dhidi ya JKT Queens, Uwanja wa Black Rhino, Karatu, Arusha na Yanga Princess dhidi ya Ceasiaa Queens, katika dimba la Uhuru, Dar es Salaam.