Tambo zimemalizwa kibabe. Ndio, kabla ya kuapigwa kwa mechi za Ngao ya Jamii ukiwa ni uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kuliibuka kelele nyingi sana.
Tambo hizi zilitoka kwa timu nne zilizopangwa kuchuana, kila upande ukitamba ni lazima ubebe taji hilo na ubishi ukamalizwa jana jioni kwenye mchezo wa fainali baina ya Simba Queens dhidi ya watetezi wa WPL, JKT Queens. Simba iliandika historia kwa kutwaa ngao baada ya kuifunga JKT kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1, huku Yanga Queens ikinyakuwa ushindi wa tatu ikiizidi ujanja Fountain Gate kwa kuifunga pia penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Michuano hiyo ilianza kupigwa Desemba 9 na kumalizika juzi Desemba 12 kwenye Azam Complex, Chamazi ikiwa ni maandalizi mapya ya msimu mpya wa Ligi ya Wanawake (WPL).
JKT ilitinga fainali baada ya kuitoa Fountain Gate kwa mabao 5-0 kwenye nusu fainali ya kwanza, huku Simba ikitinga fainali baada ya kuitoa Yanga kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika bila mabao.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa juzi jioni mara baada ya mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, kila timu ilishuka uwanjani kwa tahadhari ikiwa na kiu ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo iliyoaanzishwa kwa mara ya kwanza kwenye ligi hiyo, ikiwa na mfumo kama uliotambulishwa kwa wanaume.
Dakika 90 za pambano hilo zilishuhudiwa zikiisha kwa sare ya 1-1, JKT ikitangulia kupata bao kupitia kwa Stumai Abdallah aliyefunga kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na nahodha Jonisia Minja dakika ya 16 kabla ya Simba kuchomoa dakikia ya 24, pia kwa kichwa cha Danai BhobhoJ aliyemaliza kona ya Mwanahamis Omar ‘Gaucho’ na beki mmoja wa JKT kujichanganya na kumpa nafasi mfungaji.
Ndipo ikafuata hatua ya penalti ambapo penalti zote tano za Simba ziliwekwa kimiani na Daniela Ngoyi, Asha Mnuka, Joelle Bukuru, Ruth Ingosi na Vivian Corazone, huku za JKT zikipigwa na Ester Mabanza, Anastazia Katunzi, Christer Bahera, Donisia Minja na Happyness Mwaipaja aliyeikosa baada ya kipa wa Simba Carolyene Rufa kuicheza.
BONGE LA FAINALI
Ilikuwa fainali ya aina yake kwa timu zote mbili kuoneshana umwamba wa nani ni bora kuliko mwenzie.
Zote zilishambuliana kwa zamu na kufika katika lango la mwenzake lakini umakini wa timu zote ulizifanya kufikia hatua ya penalti.
JKT iliukamata mchezo katika dakika 15 za kwanza ikipiga pasi safi ambazo zilifikiwa vyema na utatu wa mastraika Stumai Abdallah, Jamila Rajabu na Aliya Fikiri ambao waliisumbua safu ya ulinzi ya Simba.
Simba baada ya kurudisha bao nayo haikupoa ilitengeneza nafasi nyingi ambazo hazikuzaa mabao kutokana na washambuliaji wake kuwa wazito kukimbia eneo hatari la mpinzani wakimtegemea Asha Djafar ambaye mara nyingi amejikuta akiwa peke yake ndani ya boksi na kushindwa kufanya uamuzi wa haraka.
Hivyo, kwa Simba kuchukua ubingwa iliondoka na kitita cha hundi ya Sh 5 milioni.
Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya matukio yaliyotokea uwanjani kwenye fainali hiyo.
FETTY DENSA NA STUMAI
Hapa kulikuwa na vita kali kwani wote wawili ni marafiki na wamekuwa wakicheza pamoja mpaka kwenye kikosi cha Twiga Stars.
Stumai alionekana kumsumbua sana Fetty kwa kasi yake na namna ya kumpiga chenga ya kufika eneo la ke na hata bao la kwanza lilitokea upande anaocheza Fetty.
YANGA NI ILE ILE
Baada ya kutolewa kwenye nusu fainali na Simba, Yanga ikadondokea kwenye mshindi wa nafasi ya tatu ikicheza na Fountain Gate ambayo nayo ilitolewa na JKT.
Ukiangalia msimamo wa WPL msimu uliopita, Yanga ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na nne ikiwa Foutain ndivyo ilivyokuwa kwenye Ngao.
Kuna mabadiliko kidogo kwenye kikosi cha Yanga msimu huu japo ni mapema sana kukichambua kikosi hicho, kwa kuwa kwenye mechi mbili za ngao tumeshuhudia soka la burudani kutoka kwa Wananchi.
Namna timu inavyocheza kuanzia kwa kipa wake, Safiatu Salifu kuna mabadiliko makubwa, wanacheza kama timu japo pia kuna upungufu wa namba tisa halisi ambaye ni straika wa kumalizia eneo hilo kwani timu inamtegemea Faiza Seidu ambaye wakati mwingi anashuka chini kucheza kama kiungo na winga.
Mechi mbili iliyocheza timu hiyo haijapata mabao ndani ya dakika 90 ikiilazimu kwenda kwenye penalti kuanzia mechi ya kwanza ya Simba na hii ya mwisho dhidi ya Fountain Gate.
Kwa aina hiyo ni wazi Yanga inahitaji straika halisi wa kumalizia pasi zinazotengenezwa na viungo, Precious Christopher na Saiki Atinuke.
TUZO ZATAWALA
Haukuwa usiku wa kitoto kwani kazi ambayo waliionesha mabinti hao kwenye fainali ilibidi wapongezwe kwa zawadi mbalimbali.
Mshambuliaji wa JKT, Stumai aliondoka na tuzo mbili akiwa mfungaji bora wa mashindano akifunga mabao mawili moja kwenye fainali na ile ya nusu fainali na tuzo nyingine ya mchezaji bora wa fainali.
Mbali na huyo, kipa wa Simba Carolyne Rufa aliibuka kuwa kipa bora wa mashindano baada ya kuokoa mkwaju wa penalti ya mwisho iliyopigwa na Happyness huku Vivian Corazone akibeba tuzo ya mchezaji bora wa mashindano ya ngao.
MASHABIKI SASA
Ni wazi sasa soka la wanawake linakuwa siku hadi siku ukiachana na viwango bora wanavyoonyesha wanadada hao kuna hawa wachezaji wa 12. Miongoni mwa vitu vilivyonogesha fainali ya juzi ni wingi wa mashabiki uwanjani hapo kwani walikuwa wakipongeza kila mchezaji aliyefanya vizuri. JKT sasa ndio ilivunja rekodi ukiangalia karibu robo ya uwanja walijaa mashabiki wa jeshi ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwaunga mkono wanajeshi hao wa kike.
Simba nao hawakuwa kinyonge walijitahidi kwa uchache wao kushangilia ipasavyo ili kuhakikisha timu inapata ushindi na kubeba ubingwa.
Kwa aina hiyo kuna haja ya makampuni mbalimbali na wadau kuwaunga mkono kama ilivyo kwa wanaume ili kuhakikisha soka hilo linakwenda mbali zaidi kwa kuwa tayari mashabiki wanao.
MASTAA SIMBA
Kiungo mshambuliaji wa Simba Queens, Vivian Corazone alisema ubingwa wa Ngao ya Jamii walioupata utaongeza kujiamini kuelekea msimu mpya wa ligi baada ya mwaka jana kupokwa na JKT.
“Penalti ya mwisho ina umuhimu mkubwa nadhani kocha anajua nani amalize na nani aanze hivyo tunashukuru kubeba ubingwa najua utatuongezea kujiamini zaidi na kurudisha hari yetu iliyopotea msimu uliopita,” alisema Corazone, huku beki wa timu hiyo, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ akisema ubingwa wa kwanza unawapa ishara ya kuwa wanaanza vipi msimu mpya wa Ligi Kuu.
“Timu zote zilikuwa nzuri, tulikuwa tunacheza kwa kukamiana kwa sababu tunajuana, makosa tuliyoyafanya yanatupa taswira ya namna gani tutaanza msimu,” alisema Fetty Densa.
VIKOSI
SIMBA QUEENS: Carolyene Rufa, Fatuma Issa, Dotto Evarist, Violeth Nicholaus, Ruth Ingosi, Danai Bhobho, Asha Djafar, Vivian Corazone, Elizabeth Wambui, Ritticia Nabbosa na Mwanahamis Omary.
JKT QUEENS: Naijath Abbas, Happyness Mwaipaja, Ester Mabanza, Janeth Pangamwene, Christer Bahera, Joyce Lema, Stumai Abdallah, Eto Mlenzi, Jamila Mnunduka, Donisia Minja na Aliya Fikiri.