Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Queens, Yanga Princess hakuna mbabe

Simba Queens Vs Yanga Princess Simba Queens, Yanga Princess hakuna mbabe

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Pambano la watani wa jadi kati ya Simba Queens dhidi ha Yanga Princess limekosa mbabe baada ya timu hizo kuvimbiana ndani ya dakika 90 zikitoka sare ya bao 1-1, mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Simba Queens, Charles Lukula kipindi cha pili ya kuwatoa Pambani Kuzoya na Koku Ally na kuwaingiza Vivian Corazone na Asha Jafari yaliisaidia timu hiyo kuepuka kipigo kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga Princess.

Dakika chache tu baada ya kuingia, Corazone aliipatia Simba Queens bao na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare bao 1-1.

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 45 kupitia kwa Wogu Chioma aliyefunga bao kwa kichwa akimalizia kona ya Wincate Kaali na baadae Simba kusawazisha dakika ya 59 kupitia kwa Vivian aliyepiga shuti nje kidogo ya 18 na kujaa wavuni.

Hiyo ni mechi ya tisa timu hizo zimekutana huku Simba ikishinda mara sita, sare mbili na Yanga ikishinda mara moja tu.

Yanga iliifunga Simba msimu uliopita kwa bao 1-0 lililofungwa na Clara Luvanga ambaye kwa sasa hayupo kikosini.

Opah Clement ndio kinara wa kuifunga Yanga kila wanapokutana baada ya kuifunga mabao saba kwenye mechi sita za ligi na moja kwenye mchezo wa kirafiki.

Rekodi ya kuifunga Yanga Princess mabao mengi bado inashikiliwa na Mwanahamis Omari 'Gaucho' anayecheza soka la kulipwa nchini Morocco ambaye wakati akiwa Simba Queens amewafunga watani zao wa jadi mabao 10.

2018/2019 Simba 7-1 Yanga Yanga 1-5 Simba

2019/2020 Simba 3-1 Yanga Yanga 1-5 Simba

2020/2021 Simba 0- 0 Yanga Yanga 0-3 Simba

2021/2022 Simba 4-1 Yanga Yanga 1-0 Simba

2022/2023 Simba 1-1 Yanga

Chanzo: Mwanaspoti