Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Prisons ni mechi ya mabao

NBCPL: Simba Kuanza Mzunguko Wa Pili Na Tanzania Prisons Keshokutwa Simba, Prisons ni mechi ya mabao

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Simba na Tanzania Prisons zikishuka uwanjani kesho Jumatano katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, mechi hiyo inatazamiwa kuwa na 'mvua' ya mabao kutokana na rekodi timu hizo zinapokutana.

Ndiyo. Namba hazidanganyi kwani katika misimu takribani mitano hakuna mechi iliyomalizika bila kufungana huku nyota wa Simba, Saido Ntibazonkiza akiwa kinara wa mabao aliyewafunga Wajelajela.

Katika michezo saba ya mwisho walizokutana timu hizo, Ntibazonkiza ametupia mabao matano ikiwamo matatu katika mchezo mmoja 'hat trick' wakati Wekundu wakiizamisha Prisons mabao 7-1 msimu uliopita, mechi ikipigwa Desemba 30, mwaka jana katika Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.

Mkongwe na nahodha wa Simba, John Bocco anakuwa mchezaji wa pili kufunga idadi kubwa ya mabao (matatu) walipokutana na Maafande hao kwa misimu hiyo.

TAKWIMU ZILIVYO

Katika mechi nane za mwisho msimu huu kila timu imeonyesha kasi ya ufungaji mabao japokuwa Simba imeipiga bao Prisons.

Simba ambao wamefuzu kwa mara ya nne mfululizo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Jwaneng Galax, imefunga mabao 16 kwenye michezo minane ya mwisho.

Katika michezo hiyo, Wekundu hao wameshinda mitano na sare tatu dhidi ya KMC 2-2, Asec Mimosas 1-1 na suluhu dhidi ya Jwaneng Galax wakiruhusu wavu kutikiswa mara tatu.

Kwa upande wa Tanzania Prisons katika michezo minane ambayo kocha wa sasa, Ahmad Ally ameongoza wamefunga bao kwenye michezo saba na kuwa nayo 10.

Ni mechi moja dhidi ya Ihefu iliyomalizika kwa suluhu, huku ikiwa imeruhusu wavu wake mara tano na kuwa nafasi ya sita ikiwa na pointi 24.

REKODI YAIBEBA SIMBA Katika misimu takriban mitano, Simba imeihenyesha Prisons kwani michezo 10, Wekundu hao wameshinda mitano, sare tatu na kupoteza miwili.

Utamu zaidi utakuwa katika vita ya mastaa wa timu hizo ambao wameonyesha uwezo binafsi haswa katika kuhusika kwenye matokeo mazuri ya timu.

Kwa upande wa Prisons wanawategemea straika Samson Mbangula ambaye amefunga katika michezo mitatu mfululizo akisaidiana kwa karibu na winga Zabona Hamis.

Wawili hao wamefunga mabao tisa na asisti sita ikiwa Mbangula ameingia wavuni mara tano na asisti mbili, huku Zabona akifunga mabao manne sawa na asisti.

Simba macho yatakuwa kwa Clatous Chama ambaye ameendelea kuwapa raha mashabiki wake akihusika katika michezo minne nyuma akifunga mabao matatu na asisti mbili.

Pia Babacar Sar naye hajawa mnyonge akifunga mabao matatu na asisti moja huku Saido akifunga mawili na asisti moja wakati wa mechi iliyopita dhidi ya Galaxy katika mechi ya ligi ya mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti