Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Prisons kisasi

797dddb8a94bd297fda20746e536623f Simba, Prisons kisasi

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba leo watashuka kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa kuwakabili Maafande wa Tanzania Prisons katika mchezo ambao utarajiwa kuwa wa kulipa kisasi kwa wenyeji, Simba.

Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti Simba, wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 45 katika michezo 19, wakati Prisons wakiwa nafasi ya 10 na pointi 27 katika michezo 21 waliyocheza.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga, Simba ilipoteza kwa bao 1-0, matokeo ambayo ndio yanaufanya mchezo huo wa leo kuwa wa kisasi.

Simba ambao wamerejea nchini mwishoni mwa wiki iliyopita wakitokea Sudan walipokwenda kucheza na Al Merrikh, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na kupata suluhu wataingia uwanjani leo kwa hasira katika mchezo huo ili kupata ushindi utakaowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuongoza ligi na pia kutetea ubingwa wao.

Kusuasua kwa vinara wa ligi Yanga, kunawafanya Simba kupata nguvu zaidi wakikomaa kushinda mechi zao nne za viporo ambazo zitawasaidia kukaa kileleni mwa msimamo, hivyo kwa mantiki hiyo kocha Didier Gomes, atatumia jeshi lake kamili kuhakikisha anapata pointi zote tatu bila kujali ugumu wa wapinzani wao Prisons.

Mpaka sasa taarifa ya daktari wa Simba Yassin Gembe inasema hakuna mchezaji yeyote aliyekuwa majeruhi, kitu ambacho kinampa nafasi pana kocha wao kumtumia mchezaji anayemtaka akiwepo kipa Aishi Manula ambaye aliumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania lakini kwa sasa anaendelea vizuri.

“Tunakwenda kukabiliana na timu nzuri ambayo inatumia nguvu nyingi lakini tutacheza kwa umakini ili kupata ushindi ambao utatuweka kwenye mazingira mazuri katika harakati za kuongoza ligi mipango yangu ni kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi mechi dhidi ya Al Merrikh ambao ni Jonas Mkude, Erasto Nyoni, John Bocco, Meddie Kagere na Benard Morrison,” alisema Gomes.

Kwaupande wake kocha msaidizi wa Prisons, Shaban Kazumba, amekiri kuwa mchezo utakuwa mgumu leo kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani wao Simba ambao kwa sasa wanachagizwa na ushiriki wao wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kazumba alisema wamewaanda vijana wao kupambana na kushinda mchezo huo ingawa ameeleza kuwa wachezaji wake wanalazimika kucheza kwa kujitoa kwa dakika zote 90 za mchezo ili kupata ushindi.

“Watataka kulipa kisasi sababu tuliwafunga mchezo wa kwanza lakini haitokuwa rahisi, tumekuja tukijua tunakuja kukutana na timu ya aina gani kwahiyo tupo tayari kwa mapambano ya dakika 90, najua hatupewi nafasi ya kushinda lakini tutawashangaza watu,” alisema Kazumba.

Kocha huyo alisema wachezaji wao wote wako fiti kuelekea kwenye mchezo huo na hawana presha yoyote mbele ya wawakilishi hao wa Tanzania kimataifa.

Simba pamoja na kucheza nyumbani inapaswa kuwa makini na Prisons kwani rekodi zinaonyesha msimu uliopita, pamoja na kutwaa ubingwa lakini haikupata ushindi mbele yao wala kufunga hata bao moja katika mechi zote mbili na msimu huu tayari Simba imepoteza mchezo wa kwanza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz