Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Pamba zailainishia Yanga, Azam CAF

Aziz Chama Pacome Yanga 3 Simba, Pamba zailainishia Yanga, Azam CAF

Wed, 31 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mechi za matamasha mawili ya Simba na Pamba kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi hapana shaka zitakuwa na faida kwa Yanga na Azam ambazo zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Simba na Pamba zimejikuta zikitoa mualiko wa timu mbili ambazo zitacheza na wapinzani wa Yanga na Azam kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni APR ya Rwanda na Vital'O ya Burundi.

Katika kilele cha tamasha la Simba Day, Agosti 3, Simba imepanga kucheza na APR ya Rwanda ambayo itakutana na Azam FC kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamba yenyewe imeipa mualiko Vital'O ya Burundi kwa ajili ya mechi yake ya kilele cha tamasha la Pamba Day ambayo itachezwa Agosti 10 jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Uwepo wa mechi hizo bila shaka unazipa fursa nzuri Yanga na Azam kutazama wapinzani wao hao ambao zitakutana nao katika hatua ya awali mwezi ujao.

Yanga itaanzia ugenini dhidi ya Vital'O lakini mechi hiyo itachezwa hapahapa Dar es Salaam katika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC itaumana na APR ambapo mechi ya kwanza itachezwa hapa Tanzania na marudiano yatakuwa huko Kigali Rwanda.

Mshindi wa mechi kati ya Yanga na Vital'O atakutana na mshindi wa mechi baina ya CBE ya Ethiopia na SC Villa ya Uganda na mshindi baina ya Azam na APR atacheza na Pyramids FC ya Misri katika raundi ya kwanza.

Mechi za kwanza za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa kati ya Agosti 16 hadi 18 na zile za marudiano zikipangwa kuwa kati ya Agosti 23 na 25 mwaka huu.

Msemaji wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema kuwa mkakati wao ni kuitoa APR na wamekuwa wakiifuatilia kwa muda mrefu.

"Kuanzia pale droo ilipochezeshwa na tukafahamu tutacheza na APR, tulianza kufanya maandalizi yetu ikiwemo benchi la ufundi kufanya tathmini ya ubora na udhaifu wao hivyo niseme tu kuwa msimu huu Azam FC imejidhatiti kiasi cha kutosha kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mashindano hayo," alisema Ibwe

Chanzo: www.tanzaniaweb.live