Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Pamba mtajua hamjui

Simba Mpya.jpeg Simba wanashuka Dimbani usiku wa Leo kucheza na Pamba

Sat, 14 May 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Moto utawaka. Ndoto ya wengi ya kuona mzizi wa fitina unakatwa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) imeshikiliwa na mchezo wa robo fainali ya mashindano hayo leo baina ya Simba na Pamba kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Ushindi kwa Simba bila shaka utatimiza ndoto ya wengi ya kuona nani ni mbabe msimu huu baina yao na Yanga kwani mshindi wa mechi hiyo ndio atakutana na vinara hao wa Ligi Kuu Bara katika nusu fainali itakayochezwa mwezi ujao.

Baada ya Simba na Yanga kushindwa kupata mbabe baina yao, kitendawili hicho kinaweza kuteguliwa katika hatua ya nusu fainali ambayo tayari Yanga imetangulia lakini ili hilo litimie, ni lazima Simba waitupe nje Pamba ambayo ni timu pekee ya Ligi ya Championship iliyopenya hadi hatua ya robo fainali msimu huu.

Kwenye makaratasi ni mchezo ambao Simba wanaonekana kuwa katika nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na muendelezo wa kiwango bora na matokeo mazuri ambayo wamekuwa nayo katika mashindano hayo na hata mechi za ligi kulinganisha na Pamba ambayo imekuwa na mwendo wa kusuasua kwenye Championship.

Hata hivyo, hilo halipaswi kuwafanya Simba waingie wakijiamini kupitiliza kwani hiyo inaweza kuwaondolea utulivu na umakini ambao unaweza kutumiwa vyema na Pamba kuwaadhibu.

Historia ya nyuma inapaswa kuwa fundisho kwa Simba leo mbele ya Pamba kwani imeshawahi kukutana na fedheha ya kutolewa na timu za ligi za madaraja ya chini katika nyakati tofauti tena ikiwa inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Msimu wa 2017/2018 Simba ilijikuta ikivuliwa ubingwa katika hatua ya 64 bora na timu ya Green Warriors baada ya kuchapwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia timu hizo kumaliza dakika 90 za mchezo zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kana kwamba haitoshi, msimu uliofuata baada ya huo, Simba iliondolewa tena katika hatua ya 32 bora ya mashindano hayo na timu ya Mashujaa ya Kigoma baada ya kuchapwa mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Daraja la ubora wa wachezaji baina yao na Simba linaweza kuwafanya Pamba kujaza idadi kubwa ya wachezaji katika eneo la ulinzi na kushambulia kwa kushtukiza, mbinu ambayo Simba imekuwa ikipata wakati mgumu kukabiliana nayo pindi ikutanapo na wapinzani wanaoitumia.

Simba itakuwa ikisaka taji la tatu mfululizo la mashindano hayo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita na ule wa 2019/2020 na kihistoria ndio timu iliyotwaa ubingwa wa mashindano hayo mara nyingi tangu yaliporudishwa upya msimu wa 2015/2016 ambapo imechukua ubingwa mara tatu na zinzomfuatia ni Yanga, Mtibwa Sugar na Azam FC ambazo kila timu imechukua mara moja.

Kama ambavyo wameweka historia ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza msimu huu, Pamba pia wana kiu ya kuandika historia mpya nyingine ya kuingia kwa mara ya kwanza katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Simba katika mchezo huo itawakosa Clatous Chama, Sadio Kanoute, Lwanga Taddeo Lwanga ambao ni majeruhi pamoja na Bernard Morrison ambaye ameagwa na timu hiyo.

Kocha wa Pamba, Wilbert Mweta alisema; “Hii ni mechi ya mtoano hivyo ni lazima tushinde. Tunaingia kwenye mechi hii kucheza kwa nidhamu zaidi kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele.”

“Tunajua Simba ni timu bora pia bingwa mtetezi lakini tunaamini tutafanya vizuri zaidi yao,” alisema.

Kwa upande wa kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola alieleza kuwa; “Kombe lipo kwetu na tunataka kulitetea, Pamba sio timu mbaya lakini tumejiandaa kushinda na kusonga mbele na mwisho wa siku tulichukue kombe hili kwa mara nyingine tena.”

Mbali na nusu fainali ya Yanga na mshindi wa leo Kwa Mkapa, nusu fainali ya pili itazikutanisha Azam FC na Coastal Union.

Chanzo: Mwanaspoti