Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Namungo zarejea kwa ligi

E4271d46e74c25aa68bee53d1d1b461f.png Simba, Namungo zarejea kwa ligi

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Simba na Namungo leo wana kibarua kizito cha kusaka pointi tatu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa kwenye viwanja viwili tofauti.

Simba itaikaribisha Polisi Tanzania katika Uwanja wa Benjamini Mkapa na Namungo ikitarajiwa kuchuana na Biashara United kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Timu zote mbili ziko nyuma michezo minne kwani zilikuwa zikicheza michezo ya kimataifa na zimefuzu hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba imefuzu baada ya kuitoa Plateau ya Nigeria huku Namungo ikipita kwa ushindi wa awali wa mabao 3-0 dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini baada ya mchezo wa marudiano kutochezwa kufuatia wageni wao kushindwa kulipa gharama za waamuzi na kufutwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Akizungumzia mchezo huo kocha Sven Vandenbroeck alithibitisha kukosekana kwa Rally Bwalya katika mchezo huo huku Chris Mugalu na Joash Onyango wakiwa wamepona baada ya kuumia wakiwa Nigeria.

“Mugalu na Onyango wamerudi baada ya kupata majeruhi tukiwa Nigeria. Kuna uwezekano kesho (leo) wakacheza lakini uhakika zaidi ni mchezo ujao wa Jumapili ila Larry Bwalya atakosekana kwa sababu ya matatizo ya kifamilia,” alisema Sven.

Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza michezo 11 inacheza mchezo huo ikiwa na morali wa kufanya vyema kimataifa.

Mchezo wa mwisho wa ligi ilicheza dhidi ya Coastal Union na kushinda kwa mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Simba ni bora zaidi katika safu ya ushambuliaji kwani imefunga mabao 29 ikiwa inaongoza kwa idadi mabao mengi.

Polisi tangu ipande daraja msimu uliopita kila ilipokutana na Polisi walifungwa kila mmoja kwa mabao 2-1.

Ni muhimu kwa Simba kushinda mchezo huo ili kupunguza tofauti ya pointi na Yanga ambayo imemuacha kwa pointi 11 lakini kingine ni kumpa presha Azam ambayo ipo kwenye uwezekano wa kushuka kutokana na kushindwa kufanya vizuri michezo yake iliyopita.

Lakini Polisi Tanzania siyo timu ya kubeza kwani inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 20 ikiwa imecheza michezo 14 na imekuwa ikijitajidi kupambana kupata ushindi bila kujali yuko nyumbani au ugenini.

Mchezo mwingine ni Namungo dhidi ya Biashara United utakaokuwa na ushindani kwani wote katika michezo ya mwisho walitoka sare.

Namungo walifungana bao 1-1 dhidi ya Yanga wakati Biashara United walipata matokeo kama hayo dhidi ya Azam FC.

Mchezo huo unaweza kuwa mgumu kwani Biashara imekuwa ni timu ngumu kama ilivyo Namungo na wanahitaji matokeo mazuri.

Namungo inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 15 na Biashara United inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 19 ila imecheza michezo miwili zaidi ya Namungo.

Chanzo: habarileo.co.tz