Baadhi ya mashabiki wa Simba jijini Mwanza wametoa msimamo wao kwa kusema hawana tatizo na timu kukosa mataji na kushindania nafasi ya pili Ligi Kuu msimu huu, lakini wakawapa mtihani Rais wa Heshima, Mohamed 'Mo' Dewji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah 'Tray Again'.
Msimu huu, Simba imeambulia Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano na sasa inawania nafasi ya pili na Azam FC baada ya kuyakosa mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakizungumza juzi katika hafla ya uzinduzi wa tawi la Simba Matale wilayani Magu, Mwanza lenye wanachama 72, mashabiki hao wameutaka uongozi kuondoa makandokando yanayoikwamisha timu likiwemo suala la usajili unaowafelisha.
Msemaji wa tawi hilo, Shabani Pamba, amesema; “Nawapa hongera watani kwa kuchukua ubingwa, wana Simba tujiimarishe mwakani mtani hatoboi tunaendelea kuwaamini viongozi wetu na kuendelea kuwa imara.”
Makamu Mwenyekiti wa Simba Mwanza, Salya Ludana amesema msimu huu wameteleza lakini mashabiki wasife moyo wajipange upya kwani uongozi umewahakikishia kufanya usajili wa nguvu.
“Viongozi wa juu waangalie mahali tulipoteleza kama kuna mtu amesababisha basi atolewe na kamati ya usajili kwa nini kila mara tunaletewa watu waliofeli, kwa hiyo tuwe wamoja tusajili vizuri na tuondoe makandokando,” amesema Ludana.
Mwanachama wa tawi hilo, Daud Komanya ameongeza; “Tuna imani na viongozi wetu hatuna ugomvi wowote mambo yatakwenda vizuri. Msimu huu umekuwa na changamoto nyingi kwetu tunamshukuru Mungu tutakwenda kimataifa, Simba ni kubwa Simba ni sisi.”
Kwa upande wa mwanachama mwingine, Victoria Msambili amesema; “Msimu huu pamoja na kwamba kulikuwa na changamoto lakini tunajipa imani msimu ujao tutafanya vizuri. Nafasi tuliyopo hatujaifurahia lakini daraja letu litarudi.”
Simba iliyokuwa ikishikilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo kwa sasa inafikisha msimu wa tatu mfululizo pia, bila taji hilo baada ya watani wao, Yanga kupindua meza ikiwa inashikilia pia taji la FA kwa misimu miwili kwa sasa na imeshatinga fainali ikitarajiwa kuvaana na Azam wikiendi hii.
Simba iliyopo Arusha kwa ajili ya kucheza mechi mbili za mwisho za nyumbani, ikiwamo iliyopigwa jana na kushinda dhidi ya KMC ipo nafasi ya tatu kwa sasa ikilingana pointi 66 na Azam, ila ikizidiwa mabao ya kufunga na kufungwa na keshokutwa Jumanne itamalizana na JKT Tanzania.
Hata hivyo, itacheza mechi hiyo huku ikiombea Azam ipate matokeo mabaya ugenini mjini Geita mbele ya Geita Gold, kwani iwapo wapinzani wao wakiangusha pointi na wao kushinda itamaliza ya pili, lakini kama timu zote zitashinda ni Azam itakuwa imenyakua nafasi ya pili na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ilihali Mnyama ataenda Kombe la Shirikisho ililofika robo fainali misimu miwili iliyopita.