Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Mbeya kwanza itashangaza!

Wanafainali Simba SC Simba jioni ya leo itavaana na Mbeya Kwanza

Sun, 6 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons, leo inarejea uwanjani kukamilisha mechi za duru la kwanza kwa kuvaana na Mbeya Kwanza.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza, huku kila moja ikiwa na matokeo ya kusuasua kwa siku za karibuni, jambo ambalo linawapa presha mashabiki wa klabu zote mbili kabla ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mechi tano zilizopita za ligi, Simba imeshinda michezo miwili, ikitoka sare moja na kupoteza mbili ikiwa na maana imevuna pointi saba kati ya 15 za mechi hizo, huku Mbeya Kwanza inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza haina matokeo ya kuvutia.

Timu hiyo katika mechi tano zilizopita imeshinda moja, huku ikipoteza moja na sare tatu na kuifanya ikusanye alama sita kati ya 15.

Kutokana na matokeo ya mechi hizo tano kwa kila moja, inalifanya pambano la leo kuwa la aina yake kila timu ikitaka kusaka ushindi ili kujiweka pazuri kwenye msimamo na pia kuongeza point. Mechi hiyo ni ya mwisho kwa Simba kabla ya kurejea kwenye michuano ya Caf ikicheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D na inatarajiwa kuwa wenyeji wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Kwa sasa Simba ipo nafasi ya pili Ligi kuu ikiwa na pointi 28 kutokana na mechi 14, huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu sita wakati Mbeya Kwanza ni ya 12 (kabla ya mechi za jana) ikiwa na pointi 13 na mabao 13 ya kufungwa ikifungwa 16 katika mechi 15.

Katika mechi ya leo itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku, Simba itakuwa inahitaji ushindi ili kupunguza pengo la pointi baina yake na vinara wa ligi hiyo - Yanga ambayo kabla ya usiku wa jana ilikuwa na alama 35.

Kocha wa Simba, Pablo Franco anayetumikia adhabu ya kusimamishwa mechi tatu - leo ikiwa ya mwisho, bila shaka ataendelea kuwategemea viungo ili kupata matokeo baada ya washambuliaji kuwa butu.

Katika mechi iliyopita Simba ilianza na viungo watano jambo ambalo liliwafanya kucheza mipira mingi katikati mwa uwanja isiyokuwa na faida kwani walishindwa kutengeneza nafasi za kufunga na straika wao Meddie Kagere alipokea mipira isiyokuwa eneo la hatari na mara nyingi nyuma yake alikuwa na mabeki wawili wakimkaba.

Ili kuleta mizania sawa, benchi la ufundi la Simba linahitajika kupunguza idadi ya viungo asilia na kuongeza mawinga asilia kati ya Papi Ousmane Sakho, Peter Banda na Yusuph Mhilu.

Kuanza na mawinga asili maana yake itawafungua mabeki wa Mbeya Kwanza ili kupata mianya ambayo Clatous Chama, Rally Bwalya na viungo wengine kupeleka mashambulizi hatari au kufunga wenyewe.

Uwepo wa Sakho atakuwa anakimbia kwenye nafasi na uwezo wake wa kumiliki mpira itakuwa rahisi Kagere kupata nafasi ya kufunga na kupunguza idadi ya mabeki watakaokuwa wanamkaba.

Mbeya Kwanza licha ya ugeni katika ligi, imeonekana ni timu yenye kutengeneza mashambulizi makali na kupindua meza dhidi ya wapinzani kama ilivyotokea dhidi ya Ruvu Shooting iliposawazisha jioni.

Itawategemea washambuliaji nyota akiwamo Habib Kyombo aliyetamba na Mbao kabla ya kwenda Afrika Kusini huku akiwa na bahati ya kuitungua Simba kila walipokutwana enzi hizo.

Mbali na Kyombo mwenye mabao matatu, pia inaye Willy Edger ambaye amepoa tangu alipofunga bao lake la tatu pamoja na Eliuter Mpepo aliyeongezwa dirisha dogo sambamba na Kyombo na John Mbise.

Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema wanahitaji pointi tatu katika mchezo huo ili kupunguza pengo lililopo dhidi ya watani zao - Yanga na pia kutimiza lengo la kutetea ubingwa wa ligi.

“Akili na nguvu yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda kila mechi iliyo mbele ikiwemo hii ya Mbeya Kwanza ili kuongeza pointi tulizonazo wakati huu,” alisema Matola.

Kocha wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi alisema hana presha na msimamo wa ligi kwa sababu bado kuna mechi nyingi kwenye mzunguko wa pili ambazo zinaweza kuwatoa walipo.

“Namna timu inavyocheza inajengeka na inacheza tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Kikubwa ambacho tunahitaji ni matokeo, tunawaheshimu Simba lakini tunahitaji pointi tatu dhidi yao,” alisema Maka.

WADAU WAFUNGUKA

Nyota wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe na Boniface Pawasa, wanaamini ushindi ambao timu hiyo imeupata mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons umerejesha morali na ari ya kujiamini kwa wachezaji.

Ulimboka alisema: “Kitendo cha kuifunga Prisons naamini kimerejesha morali kwa wachezaji hivyo tutegemee kuona wakifanya vizuri kwenye michezo ijayo.”

Naye Pawasa alisema: “Walipambana na kupata matokeo dhidi ya Prisons kwa kiasi fulani ushindi huo utawasadia kuinua hali ya kujiamini kwa mchezaji mmoja mmoja.”

MECHI NYINGINE

Katika michezo mingine ya Ligi Kuu Bara leo, Geita Gold wataikaribisha Polisi Tanzania, wakati Namungo watakuwa Lindi kucheza na Mtibwa Sugar.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz