Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Kagera Sugar vitani leo

9fd8c2c8e4040efb37be318d5bc55616.jpeg Simba SC wana kibarua kizito mbele ya Kagera leo

Sat, 18 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kocha Msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola, amesema kuwa anaamini kikosi chake kitaendeleza wimbi la ushindi watakapokutana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu katika uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba leo. Simba inaingia katika mchezo huo huku robo tatu ya kikosi ikiwa imekumbwa na ugonjwa wa mafua na kikohozi.

Mabingwa watetezi wanashuka kuwakabili Kagera Sugar, wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi wa bao 2-0, walipokutana mara ya mwisho kwenye Uwanja huo. Akizungumza na gazeti hili jana Matola alisema, anaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na tabia ya baadhi ya timu kuweka nguvu kubwa pindi inapocheza na bingwa mtetezi, lakini kwa maandalizi waliyoyafanya anaamini wanaenda kushinda mchezo huo.

“Kila mchezo ulio mbele yetu ni mgumu msimu huu malengo yetu ni makubwa tunahitaji kuendeleza wimbi letu la kutetea mataji tuliyoshinda jambo ambalo sio rahisi iwapo kama hatutatimiza majukumu yetu,”. “Tunawaheshimu wapinzani wetu wana timu nzuri lakini sisi ni bora kuliko wao, nawaomba mashabiki waje kwa wingi kutusapoti katika mchezo huu japokuwa tuna wachezaji majeruhi Sadio Kanoute, Chris Mugalu na Thadeo Lwanga,” alisema Matola.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza, alisema kuwa wanaingia kwenye mchezo wa leo wakijua fika kuwa wanaenda kukutana na timu bora hivyo lazima watakutana na wakati mgumu lakini amewaandaa vijana wake ili kuhakikisha pointi tatu zinabaki nyumbani.“Ni mchezo mgumu kutokana na aina ya wapinzani wetu japokuwa tuko nyumbani tunapaswa kushinda na kuwapa furaha mashabiki wetu na kuongeza ari upambanaji kikosini,” alisema Baraza.

Michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo ni Mtibwa Sugar dhidi ya KMC katika Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro, nao Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City, kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo Simba, imezindua rasmi kampeni yake ya kuchangia ujenzi wa Uwanja wao utakaokuwa ukitumika kwa michezo yao ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000, jambo ambalo tayari mwekezaji wa timu hiyo Mohamed Dewji ‘Mo’ aliahidi kutoa kiasi cha Sh bilioni mbili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz