Kesho Jumamosi ni siku ya wenye nchi wanaotembea na kauli mbiu ya Vita ya Kisasi wakati itakapoikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika pambano la kufungia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika litakalopigwa Kwa Mkapa.
Ndio siku inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, hususani Wanamsimbazi wenye hamu ya kuona Simba ikilipa kisasi kwa Jwaneng na kutinga robo fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi B.
Ni turufu ya mwisho kwa Simba kwani inahitaji ushindi wa aina yeyote ili kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kutokana na namna kundi B lilivyo.
Katika kundi hilo, tayari Asec Mimosas imefuzu ikiwa na alama 11 hivyo imebaki nafasi moja inayowaniwa na Simba, Wydad Casablanca na Jwaneng Galaxy.
Simba na Wydad zinalingana alama (6), huku Jwaneng ikiwa na nne hivyo endapo Wanamsimbazi hao watashinda watakuwa wametinga moja kwa moja bila kujali matokeo ya Wydad na Asec kwani Wekundu wa Msimbazi wanaipiga bao Wydad kwenye matokeo ya jumla walipokutana (head to head), ubao ukisoma 2-1, baada ya Wydad kuanza kwa kushinda 1-0, nyumbani na Simba kulipa kisasi kwa Mkapa iliposhinda 2-0 kwa mabao ya Willy Onana.
Kutokana na ukubwa na thamani ya mechi ya leo, Simba kupitia kwa ofisa habari wake Ahmed Ally wameipachika jina la ‘Vita ya Kisasi,’ mechi hiyo.
Ni kisasi kwelikweli kwani Jwaneng mwaka 2021 iliiondosha Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika tena kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya kuichapa mabao 3-1, ilihali Mnyama alikuwa ameshinda 2-0 ugenini. Hapo ubao wa matokeo ya jumla ukasoma Simba 3-3 Jwaneng lakini Wabotswana hao wakasonga mbele kwa faida ya bao la ugenini na Simba kutupwa nje ya michuano hiyo.
Matokeo hayo yalimuuma kila mwanasimba huku maumivu zaidi ikiwa ni kuondoshwa kwa kuichapa kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao mara nyingi timu hiyo imekuwa ikifanya balaa bila kujali inacheza na timu gani. Hapo Jwaneng ilichana mkeka. Siku zimeenda na kwa mara nyingine timu hizo mbili leo zitakutana kwenye ardhi ileile ambayo Jwaneng iliacha majonzi kwa Simba. Je Mnyama atalipa kisasi au Jwaneng ataendelea kuchana mkeka?
Wakati ukiendelea kujiuliza kuhusu hilo, Mwanaspoti kupitia makala hii linakuletea kisasi halisi kitakavyokuwa baina ya wachezaji wa timu zote mbili ambao walikuwepo katika mechi ya Oktoba 21, 2021 na hadi sasa wapo kwenye vikosi hivyo. Simba wamebaki tisa huku Jwaneng wakisalia sita.
SIMBA AISHI MANULA Huyu ndiye kipa wa Simba aliyeokota nyavuni mpira mara tatu kila baada ya Jwaneng kucheka na nyavu.
Mabao yote yale yaliyoiondosha Simba 2021 alifungwa Manula na sasa atakuwepo kikosini hapo.
Huenda Manula akadaka kwenye mechi hii kwani ndiye alidaka mechi iliyopita ya Simba kimataifa dhidi ya Asec na kama ikiwa hivyo basi atakuwa na kumbukumbu nzuri na Wabotswana hawa, hivyo ataamua kulipa kisasi ama kuendelea kuwa ‘chujio’.
SHOMARI KAPOMBE Huyu ni beki wa kulia wa Simba aliyecheza dakika 90 zote za mechi ile ambayo Mnyama alilala kwa mabao 3-1, mbele ya Jwaneng mwaka 2021.
Kapombe hadi sasa ndiye chaguo la kwanza la Simba katika eneo hilo na mechi iliyopita dhidi ya Asec alicheza eneo hilo. hii ni mechi yake ya kisasi ama kuendelea kudhalilika mbele ya Jwaneng.
MOHAMED HUSSEIN Mwaka wa 10, sasa staa huyu maarufu kwa jina la ‘Tshabalala’, anakula mbavu ya kushoto ya Simba bila upinzani.
Alikuwa uwanjani wakati Simba inadundwa 3-1 na Jwaneng mwaka 2021, Tshabalala atakuwepo tena kwenye mechi hii huku akiwa na asilimia kubwa za kuvaa kitamba cha unahodha wa Wanalunyasi.
Ni siku yake kulipa kisasi ama kuendelea kuwa mnyonge.
HENOCk INONGA Beki kiongozi wa Simba, Inonga naye alikuwa miongoni mwa walinzi waliokuwa kwenye Uwanjani wakati Jwaneng inadumbukiza mpira mara tatu kwenye nyavu za Simba. Hakumlinda vyema Manula.
Hadi sasa bado yupo Msimbazi na anaenda kukutana tena na Jwaneng akiwa ameimarika zaidi, ni wakati wake kulipa kisasi.
SADIO KANOUTE Mwamba huyu alianza kwenye mechi ile ambayo Simba ilikufa kwa mabao 3-1 mbele ya Jwaneng mwaka 2021.
Kanoute hadi sasa bado yupo Simba hivyo kama akipata nafasi, mchezo wa leo utakuwa wa kisasi kwake.
ISRAEL MWENDA Jasho lilimtoka pia Mwenda wakati Jwaneng inashinda 3-1 kwa Mkapa mwaka 2021. Hakuondoka Simba na sasa ameimarika zaidi. Mechi hii itakuwa na kumbukumbu ya aina yake kwake.
MZAMIRU YASSIN Kiungo huyu alikuwa benchi wakati Jwaneng wanahitimisha safari ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2021.
Hakupata hata dakika moja ya kucheza ili kuipambania timu yake. Siku zimeenda na Mzamiru bado yupo Simba. Hii ni mechi yake kuonyesha kazi.
KENNEDY JUMA Beki huyu pia alikaa benchi kwa dakika zote 90 na kushuhudia chama lake likibugizwa mabao 3-1, ilimuuma lakini hakupata nafasi ya kuingia kupambania timu yake.
Huu ni muda wake wa kufanya hivyo kama atapata nafasi kwani bado yupo Msimbazi.
JOHN BOCCO Kisasi kamili kipo kwa Bocco. Nahodha wa Simba katika mechi ile ambayo timu yake ilifungwa 3-1, lakini hadi leo ndiye nahodha wa Simba.
Haitakuwa vyema kwake kuhadithia wajukuu zake siku akistaafu kuwa alifungwa mara mbili na Jwaneng tena kwa Mkapa wakati akiwa nahodha wa Simba. Hiki ni kisasi kwake.
JWANENG: MOAGI SECHELE Huyu ni beki wa kulia wa Jwaneng, alicheza dakika 90 zote wakati chama lake linaiua Simba 3-1 kwa Mkapa mwaka 2021.
Bado yupo kikosini hapo na ni staa wa kikosi cha kwanza cha Wabotswana hao wenye alama nne baada ya mechi tano.
GILBERT BARUTI Huyu ni kiungo wa juu wa Jwaneng, aliisumbua sana ngome ya ulinzi ya Simba na kuisaidia timu yake kupata mabao 3-1, mwaka 2021.
Hadi sasa bado yupo kikosini hapo akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza. Ni wakati wake kukutana tena na Inonga na Kanoute.
THABO LEINANYANE Dakika 90 za mechi ile ya 2021, huyu ndiye alikuwa kitasa cha mwisho kwa Jwaneng. Simba ilifurukuta lakini harakati zote zikaishia kwa mwamba huyu. Hadi sasa yupo kikosini hapo na ndiye beki kiongozi katika safu ya ulinzi ya Jwaneng.
LESEGO KEREDILWE Huyu ni beki mwingine wa kati anayeunda pacha na Thabo. Wote hawa walikuwepo wakati Jwaneng inaichapa Simba 3-1. Kwa pamoja walifanya kazi kubwa ya kuidhibiti Simba.
Siku zimeenda lakini bado Lesego amesalia Jwaneng akiunda ukuta na Thabo. Ni pacha imara ambayo Simba inatakiwa kuivunja kwa hesabu kali.
THABANG SESINYI Moja ya washambuliaji hatari katika kikosi cha Jwaneng kwa muda mrefu sasa. Thabang alianza kwenye mechi ile ya mwaka 2021, na sasa ndiye mshambuliaji kinara wa Jwaneng. Inonga, Kapombe, Manula na Tshabalala wanamkumbuka.
WENDELL RUDATH Katika mechi ile ya mwaka 2021, Simba ndiyo ilianza kupata bao dakika ya 41 kupitia kwa Rally Bwalya lakini dakika ya 46 bao hilo lilirudi kupitia kwa mwamba huyu.
Wendell hakupoa kwani dakika ya 60 aliitungua tena Simba na ubao kusoma 1-2 kabla ya Gape Mohutswa kuifungia Jwaneng bao la tatu dakika ya 86 na mechi kuisha.
Moto utawaka kesho. Kiufupi mwamba huyu anaijua vyema Simba na bado yupo kikosini Jwaneng akiwa winga tegemeo. Manula anamkumbuka haswaa. raundi hii itakuwaje? tusubiri tuone.