Juzi ilifanyika droo ya makundi na ratiba ya mashindano ya Get International kwa timu za wanawake yatakayofanyika Dodoma, lakini wababe wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), JKT Queens na Simba Queens zimechomoa kushiriki zikiiacha Yanga Princess na nyingine kujitosa.
Mashindano hayo yanayoendeshwa na klabu ya Fountain Gate ikiwa ni msimu wa tatu, awali ilielezwa yangeshirikisha klabu 12, lakini kabla ya droo hiyo zilizokuwa zimethibitisha kushiriki zilikuwa ni nane.
Klabu zilizothibitisha kushiriki ni Yanga Princess, New Generation ya Zanzibar, Fountain Gate Princess, Bunda Queens, CFC Aman kutoka DR Congo, Baobab Queens na Alliance Queens.
Kocha Mkuu wa JKT Queens, Esther Chabruma alisema hawatashiriki kutokana na wachezaji 16 wa kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa WPL na Klabu Bingwa ya Cecafa kuitwa timu ya taifa ‘Twiga Stars’ inayojiandaa na michuano ya kimataifa.
“Tulitamani kushiriki, lakini tukiangalia karibu kikosi kizima kimeiwa timu ya taifa kwahiyo inakuwa kushiriki kwasababu wachezaji wote muhimu wanalitumikia taifa.” alisema Chabruma
Kwa upande Simba Queens pia wameshindwa kushiriki na sababu ikielezwa kuwa ni wachezaji wa timu hiyo kutumikia timu zao za taifa.