Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Do or Die

Simba Do Pic Data Simba Do or Die

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SUALA la Simba kutawala Afrika liko mikononi mwao na mpira uko miguuni mwao. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu nafasi ya miamba hiyo ya soka nchini kuamua hatima yao ndani ya siku 26 zijazo.

Simba ipo katika nafasi nzuri ya kutimiza lengo la kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na lile la Kombe la Shirikisho la Azam msimu huu lakini mbele yake ina kiunzi ambacho ikifanikiwa kukiruka itakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanya hivyo.

Kibarua hicho kilicho mbele ya Simba ni mechi nne za Ligi Kuu, mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho la Azam ambazo italazimika kuzicheza ndani ya muda mfupi wa siku 26 pasipo kupata muda wa kutosha wa kupumzika.

Kutokana na muda mfupi wa kujiandaa kutoka mechi moja hadi nyingine na ubora wa timu hizo pamoja na ushindani ambao zimekuwa zikiutoa, ni wazi kwamba benchi la ufundi la Simba litakuwa linaumiza kichwa kuona ni kwa namna gani kikosi chake kitaweza kuhimili mechi hizo pasipo kuathirika upande mmoja au katika mashindano yote.

Ikiwa na mapumziko ya wastani siku tatu kutoka mechi moja hadi nyingine yatakayohusisha pia safari kadhaa za kutoka eneo moja hadi jingine, Simba inapaswa kuchanga vyema karata zake katika mechi hizo ili iweze kutimiza hesabu zake za kufanya vizuri katika mashindano hayo na kinyume chake itageuka kuwa msindikizaji. Yani ni ‘do or die’ kwao.

Hesabu hizo ngumu kwa Simba zitaanzia Aprili 3 wakati watakapoikaribisha AS Vita Club ya DR Congo katika mchezo wa raundi ya tano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao Simba inahitajika kupata ushindi au sare ili iweze kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Ikiwa itapoteza mechi hiyo dhidi ya AS Vita Club nyumbani, Simba itajiweka katika nafasi ngumu ya kufika robo fainali kwani baada ya hapo italazimika kusafiri na kwenda Cairo, Misri ambako itakuwa na mechi ngumu ya ugenini dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya huko itakayochezwa Aprili 9.

Kama Simba itashinda dhidi ya AS Vita ama kutoka sare na kisha ikapata matokeo kama hayo dhidi ya Al Ahly ugenini, itamaliza ikiwa kinara wa kundi A.

Baada ya kumalizana na Al Ahly, Simba itarudi nyumbani ambako itakuwa na kibarua cha kucheza mechi mfululizo za Ligi Kuu huku pia wakiwa na mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Kagera Sugar.

Wakitoka kucheza na Al Ahly, Simba wakitua tu Dar es Salaam watalazimika kufunga safari nyingine hadi Kagera ambako Aprili 14 watakuwa na mechi ngumu ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar na baada ya hapo watarejea nyumbani kuikabili Dodoma Jiji, Aprili 18.

Aprili 25 Simba itakuwa tena nyumbani kucheza na Coastal Union na siku tatu baadaye itaikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu itakaocheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Lakini pia ndani ya muda huo wa siku 26, Simba italazimika kukutana na Kagera Sugar nyumbani katika mechi ya hatua ya 16 ya Kombe la Shirikisho la Azam ambayo bado haijapangiwa baada ya kuahirishwa kutokana na ushiriki wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na awali ilipangwa kuchezwa Aprili 4.

Kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa alisema kuwa ni ratiba ngumu lakini watahakikisha wanatafuta mbinu za kukabiliana nayo.

“Mechi ni nyingi na tutacheza ndani ya muda mfupi lakini hilo halipaswi kuwa kisingizio. Tunatakiwa kujipanga vizuri tucheze hizo mechi na tuweze kufanya vyema. Jambo la msingi ambalo tunatakiwa kulifanya ni kujiandaa vizuri kwani tuna kikosi kipana kinachoweza kumudu mechi hizo.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz