Simba leo Jumapili inashuka kwenye dimba la Benjamin Mkapa kupepetana na Coastal Union ya Tanga, huo ukiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara mzunguko wa nne.
Simba, ambao ndio mabingwa watetezi wa taji hilo, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi hafifu wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania Jumatano iliyopita, huku Coastal nayo ikitoka kupoteza kwa idadi kama hiyo mbele ya Maafande wa Ruvu Shooting.
Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa kwa wenyeji Simba kutokana na uwepo wa kocha mpya, Thiery Hitimana ambaye huo utakuwa mchezo wake wa pili akiwa Kocha Mkuu baada ya kujiuzulu kwa Mfaransa Didier Gomes.
Hitimana aliyewatupia lawama mashabiki wa timu yake kwamba wao ndio waliosababisha presha kwa wachezaji hata kupata wakati mgumu kwenye mechi iliyopita na Polisi, anatarajia kufanya mabadiliko ya kikosi kwa kuweka sura mpya na zile zilizoanzamchezo uliopita, lakini hata mfumo wa uchezaji huenda akabadili.
Kwenye nafasi ya ulinzi wa kati huenda Kenndy Juma au Erasto Nyoni mmoja wao huenda akaanza kuchukua nafasi ya Joash Onyango kwenye eneo la kiungo, Bernard Morrison naye huenda akaanza sambamba na Larry Bwalya ili kutengeneza nafasi kwa washambuliaji Meddie Kagere na John Bocco, ambaye naye leo anarajiwa kuanza katika mfumo wa 4-4-2.
Kocha Hitimana amesema hakuna mchezaji aliye majeruhi kwenye kikosi chake na maandalizi yao ni mazuri
kuelekea mpambano huo, ambao alisema utakuwa na ushindani ingawa ana uhakika wa kushinda kutokana na presha kuondoka kwa wachezaji wake.
“Maandalizi yetu yamekwenda vizuri mpaka sasa vijana wangu wote wapo sawa kiafya na kiakili pia najua nakwenda kukutana na Coastal ni timu nzuri, inafundishwa na kocha mwenye uwezo mkubwa, lakini tumejipanga kuhakikisha tunautumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani,” amesema Hitimana.
Kwa upande wake, kocha wa Coastal Union, Melis Medo amesema pamoja na kikosi chake kuendelea kuimarika siku hadi siku, amekiri kwamba mchezo huo ni mgumu sana kwao na hiyo inatokana na kucheza na mabingwa watetezi.
Amesema wataingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu Simba kutokana na ubora wao, lakini wakati huo huo watakuwa wakifanya mashambulizi ya kushitukiza akiamini wanaweza kupata mabao mbele ya miamba hiyo ya soka nchini.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikijivunia ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tazania Bara msimu wa 2020/21 uliopigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.