Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam ni mabao tu

Sakho Vs Azam Simba, Azam ni mabao tu

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Uwanja wa Benjamin Mkapa, leo Alhamisi kuna kazi moja tu. Mabeki wa Azam FC na Simba kuwa na kibarua cha kula sahani moja na washambuliaji wa timu hizo, ili kuepuka aibu kwani upande utakaozubaa huenda ukapigwa nyingi kama utani.

Ndio, Azam na Simba zinavaana kuazia saa 1:00 usiku kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, huku rekodi zikionyesha safu za mbele za timu hizo zikiwa na moto na kuwapa kazi ngumu mabeki wa timu hizo kuwa na kibarua cha kuwakaba wasilete madhara kwa makipa.

Safu ya ushambuliaji ya Simba chini ya Moses Phiri na Clatous Chama, imekuwa na mwendelezo mzuri wa kupata mabao kwenye kila mchezo kati ya sita iliyocheza ikifunga 12 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara tatu tu, wakati safu ya ulinzi ya Azam imeruhusu mabao matano na kufunga saba.

Simba itakuwa ugenini tena dhidi ya Azam ikiwa na kumbukumbu ya sare ya 1-1 dhidi ya Yanga, huku wenyeji wao wakitoka kuchapwa mabao 2-1 na KMC, ambayo usiku wa jana ilikuwa ikimalizana na Yanga kwenye uwanja huohuo.

Hii ni mechi kubwa na yenye mvuto kwa mashabiki kutokana na upinzani uliopo, lakini rekodi zikiibeba Simba mbele ya wapinzani wao hao na kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Juma Mgunda akikiri ana dakika 90 nyingine ngumu leo kutokana na mastaa wake kutoka kutumia nguvu nyingi dhidi ya watani wao huku akisisitiza kuhitaji pointi tatu na mabao zaidi ya mawili kujiweka sawa.

“Natambua wachezaji wangu wametoka kucheza dakika 90 ngumu dhidi ya Yanga na wametumia nguvu nyingi na tunakutana na Azam ambayo ni timu nzuri, ila naliamini jeshi langu kwani liko vizuri kwenye utimamu wa mwili naamini watafanya vizuri,” alisema Mgunda na kuongeza;

“Ugumu utakuwepo kwa sababu tunakutana na timu nzuri na shindani lakini nimewaandaa vizuri wachezaji wangu na wao wanatambua nini tunakitaka ili kuendelea kuongoza msimamo sio pointi tatu tu pia tunahitaji idadi kubwa ya mabao ambayo yataongeza idadi ya ushindani.”

VITA YA MAKOCHA

Mgunda ana kaimu nafasi ya ukocha mkuu wa Simba na ameiongoza timu hiyo katika mechi saba za kimashindano na mbili za kirafiki na kushinda nane huku akipata sare moja dhidi ya Yanga

Kocha Kally Ongala aliyewahi kuzichezea Azam na Yanga miaka ya nyuma, yupo na Azam kitambo kama kocha wa washambuliaji na amekabidhiwa timu baada ya Denis Lavagne, alihusika kwenye maandalizi tangu timu iwe kwa Abdihimid Moallin.

Mechi ya Simba haitakuwa ngeni kwake kwani hata walipoibana Yanga kutoka sare ya 2-2 alikuwa kwenye benchi akikaimu ukocha mkuu. kabla ya Lavagne kuajiriwa na mchezo uliopita wa kipigo cha 2-1 dhidi ya KMC alikuwa benchi na sasa anaingia akiwa na kazi ya kuizuia Simba ya Mgunda isilete madhara zaidi.

Rekodi zinaonyesha katika mechi saba Azam imeshinda mara tatu, sare mbili na kupoteza miwili ikishika nafasi ya sita na pointi 11 na mchezo wa mwingo baina ya timu hizo uliopigwa Kwa Mkapa Januari Mosi, Azam ililala 2-1 kwa mabao ya Sadio Kanoute na Pape Ousmane Sakho wakati lile la Azam lilifungwa na Mzambia, Rodgers Kola. Nyota hao wote wapo na wanaweza kuliamsha leo.

Azam iliifunga Simba mara ya mwisho kwenye Ligi Kuu ilikuwa Januari 28, 2017, iliposhinda bao 1-0 lililofungwa na John Bocco ambaye kwa sasa anakipiga Simba akiwa pia nahodha wa timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti