Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam baba lao Ligi Kuu

7cfbce498aa4f2ff824061c8e478aef8 Simba, Azam baba lao Ligi Kuu

Sat, 3 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

S IMBA na Azam FC ndio baba lao, unaweza kusema hivyo, kutokana na takwimu za mzunguko wa nne kuonesha kila mmoja ubora wake katika kutupia mabao na mwingine akiwa na ukuta wa chuma.

Hao ndio vinara wakifuatiwa na wengine lakini pia, wapo ambao hali zao ni mbaya yaani ukikutana nao ukuta wao unavuja kiulaini.

SAFU BORA YA USHAMBULIAJI

Mabingwa watetezi Simba wana safu bora ya ushambuliaji ikiongoza kwa kufunga mabao mengi katika michezo minne iliyopita.

Mpaka sasa wekundu hao wamefunga mabao 10 ikiwa ndio timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kuliko nyingine yoyote.

Ikiwa na maana kubwa kwa wapinzani kuwa makini pindi wanapokutana kwani wakizubaa watanyweshewa mvua ya mabao. Safu yao ya ushambuliaji inaongozwa na Meddie Kagere na Chris Mugalu na viungo wao moto kama Cleatus Chama na Mzamiru Yassin, ambao kila mmoja ametupia mabao mawili.

Hao ni baadhi ya wanaowakilisha vyema ila wana wachezaji wengi wazuri waliotupia bao moja na kuna ambao pia ni hatari zaidi katika kuchangia mabao kwa maana ya kutoa pasi zilizoleta matunda kama Luis Miquissone, John Bocco, Bernard Morrison na wengine.

Mbali na Simba, KMC ni timu ya pili kwa ubora hasa katika safu ya ushambuliaji ikifunga mabao manane.

Wachezaji wao wanaoongoza kwa kutupia mabao ni Reliant Lusajo na Hassan Kabunda kila mmoja mabao mawili. Timu nyingine inayojitahidi kufunga mabao ni Azam FC, Polisi Tanzania waliofunga matano na Yanga manne ingawa mabingwa hawa wa kihistoria wana ubutu kwenye safu ya ushambuliaji kwani mabao yao mawili yamefungwa na beki na mengine kiungo na mshambuliaji.

SAFU BORA YA ULINZI

Katika safu bora ya ulinzi wanalambalamba wa Chamazi wameanza vyema kwasababu ndio timu pekee haijaruhusu bao kwenye nyavu zake.

Azam FC licha ya kwamba ndiye kinara kwa pointi 12 ikimuacha Simba na Yanga kwa tofauti ya pointi mbili imefunga magoli matano ila hakuna bao hata moja ililoruhusu kufungwa.

Hiyo ina maana haifungwi kiurahisi inaongozwa na golikipa David Kissu aliyekuwa bora kuchomoa mipira hatari iliyokuwa inaelekea langoni kwake. Pia, beki Yakubu Mohamed kwa ubora hadi kuchangia kuitwa kwenye timu yake ya taifa ya Ghana.

Wengine kwenye safu ya ulinzi kuna Bruce Kangwa, Nicolaus Wadada, Abdallah Heri ambao wote wameonekana kuwa moto pale wanapopata nafasi katika mechi tofauti zilizopita.

Timu nyingine inayofuatia kwa ukuta bora ni Yanga baada ya kuruhusu kufungwa bao moja kwenye nyavu zake. Safu ya ulinzi ya Yanga inaongozwa na kipa Metacha Mnata, beki bora Lamine Moro ambaye sio tu analinda bali amefunga mabao mawili.

Wengine bora ni Bakari Mwamnyeto na Shomari Kibwa kila mmoja akifanya majukumu yake vizuri.

Timu nyingine iliyokuwa ngumu katika ukuta wake ni Ruvu Shooting imeruhusu bao moja ingawa katika safu ya ushambuliaji wanaonekana kuna udhaifu kwani wamefunga bao moja katika mchezo waliomfunga Gwambina bao 1-0, wakifungwa mmoja bao 1-0 huku mingine wakitoka suluhu.

REKODI MBOVU

Ukiachana na hao waliofanya vizuri kuna ambao wanataabika wakishindwa kufunga mabao lakini pia, wakiruhusu kufungwa mabao mengi ukilinganisha na wengine.

Mpaka sasa Mbeya City ndio timu iliyoruhusu kufungwa mabao mengi yaani saba ikionesha dhahiri namna ilivyo na safu mbovu ya ulinzi kuanzia kwa golikipa wao hadi mabeki.

Timu hiyo licha ya kufanya usajili ikitoka kutaabika msimu uliopita imeshindwa kuendana na ushindani katika mechi nne zilizopita.

Unaweza kusema ni miongomi mwa timu mbili hazijafunga bao hata moja ikiwa na safu mbovu ya ushambuliaji pia. Kocha wa kikosi hicho Amri Said alisema hivi karibuni kuwa anashangaa wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga ila wachezaji wanapokuwa eneo la hatari wanakosa utulivu na kuahidi kukibomoa kikosi chake na kukitengeneza upya.

Pengine kuanzia mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons wakaja kivingine na kuwashangaza watu. Sio hao tu, bali kuna Gwambina. Hii ni timu iliyopanda Ligi Kuu msimu huu ikitokea daraja la kwanza.

Mpaka sasa timu hii imeshindwa kuendana na kasi ya ushindani baada ya kutoshinda mchezo wowote ikiwa na pointi moja iliyoambulia katika mchezo mmoja waliopata sare ya bila kufungana.

Safu yake ya ulinzi imeruhusu kufungwa mabao matano na kwa hivyo, wana kazi kubwa mbele kama hawatabadilika.

Wengine wanaotaabika ambao bado wanahitaji kupambana zaidi ni Ihefu iliyofungwa mabao matano na kufunga mawili ikiwa imeshinda mchezo mmoja pekee, Mwadui ilifungwa mabao manne na kufunga matatu na kushinda mchezo mmoja.

Kuna Coastal Union iliyofungwa mabao matatu, ubovu wake upo katika safu ya ushambuliaji iliyofunga bao moja katika michezo minne, Kagera Sugar na Ruvu zilizofunga bao moja kila mmoja ila ukuta wao bado ni mgumu kufungika kiurahisi mmoja akiruhusu bao moja na mwingine mawili.

JKT Tanzania imefunga mabao mawili na kufungwa manne ikimaanisha safu ya ulinzi sio imara sana na vile vile, ushambuliaji bado wana kazi kubwa ya kutafuta mabao mengi.

Zipo timu kama Mtibwa, Namungo, Biashara na Dodoma ambazo uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa yanafanana au kutofautiana kidogo.

Kuta zao ni ngumu kidogo na kadhalika washambuliaji wana kazi kubwa ya kupambana ya kutafuta dawa ya kufunga.

Bado ni mapema na ligi inaendelea kila mmoja anaweza kubadilika kwani makocha wamekuwa wakisomana mbinu na huenda wengine wakabadilika na kuwa bora kama watarekebisha mapungufu yao.

Chanzo: habarileo.co.tz