Simba imepangwa kucheza na Al Ahly kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Hii itakuwa mara ya saba kwa Simba kukutana na Al Ahly katika miaka sita ya hivi karibuni na rekodi zinaonesha hakuna mnyonge baina ya timu hizo hivyo mechi za duru hii zitakuwa za kuamua nani mbabe zaidi.
Mastaa wengi wa vikosi hivyo wanajuana na wamewahi kukutana katika mashindano haya sambamba na yale ya African Football League yaliyopigwa mwaka jana kwa mara ya kwanza. hizi mbili zitakuwa za ubabe zaidi.
Katika mechi sita zilizopita, wababe hao wawili walipokutana, kila timu imeshinda mara mbili na kutoa sare mara mbili kiufupi hakuna timu iliyofungwa nyumbani kwake.
Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea ubabe wa mechi hii utakapokuwa baina ya wachezaji wa vikosi vyote viwili.
AYOUB- EL SHENAWY
Hapa ni vita ya Waarabu. Kipa wa Simba Mmorocco Ayoub Lakred ameonekana kuleta mapinduzi kikosini hapo kwa kumpiku aliyekuwa kipa namba moja wa muda mrefu Aishi Manula.
Katika mechi mbili zilizopita timu hizo zilipokutana kwenye African Football League na zote kumalizika kwa sare, Simba ilimtumia kipa Ally Salim huku Ahly ikikomaa na El Shenawy.
Ubora wa sasa wa Ayoub utakuwa changamoto kubwa kwa washambuliaji wa Ahly kupata bao lakini pia uzoefu na ubora wa El Shanawy itakuwa changamoto kwa Simba na mbabe zaidi anaweza kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainali.
KAPOMBE VS EL SHAHAT
Hapa pia hakuna jpya wawili hawa wote wamekutana kwenye mechi mbili zilizopita hivyo mechi zijazo ni za kuamua nani mbabe.
Kapombe akiwa ni bora kwenye kupanda na kushambulia, Hussein El Shahat amekuwa bora kwenye kasi na kushambulia. Upande huu atakayekuwa mbabe na mbunifu zaidi ataweza kushinda mechi hii.
ZIMBWE VS TAU
Eneo lingine ambalo watakutana wazoefu ni upande wa huu ambapo Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ atakutana na Percy Tau.
Wawili hawa wamekutana zaidi ya mara tatu kwenye michuano ya CAF na kila mmoja kufanya vyema kwa upande wake kwani hadi sasa Tau raia wa Afrika Kusini ana mabao manne kwenye Ligi baada ya mechi nane huku Zimbwe Jr akiwa ni beki mzoefu na mwenye ubora wa kupanda na kushuka akiwa na Asisti tatu hadi sasa.
CHE MALONE VS MAGDY
Beki wa Simba Che Malone anaweza kukutana na usumbufu wa kiungo wa Al Ahly, Mohamed Magdy maarufu Ashfa ambaye mara kadhaa hucheza namba 10 kikosini hapo.
Hata hivyo wawili hawa wanajuana vyema kwani walikutana kwenye mechi mbili za AFL na kutoana jasho na huu ni muda wa mmoja wao kuonyesha ubabe kwa mwenzake.
INONGA VS MODESTE
Straika kinara wa sasa wa Al Ahly ni Mfaransa Anthony Modeste ambaye kwa sasa ameanza kujipata kikosini hapa.
Mkali huyu aliyewahi kukipiga Bordeaux, Blackburn Rovers na Borussia Dortmund atakuwa na kazi kubwa ya kumpita beki kisiki wa Simba, Henock Inonga Bacca mwenye kiwango bora kwa sasa.
SARR VS ATTIA
Ubabe mwingine utakuwa baina ya viungo Babacar Sarr wa Simba na Marwan Attia wa Ahly ambao wote wamekuwa na ubora mzuri.
Kama watapata nafasi kwenye vikosi vyao itakuwa mara ya kwanza kukutana na hapo ndipo kila mmoja atataka kumvimbia mwenzake na burudani itaanzia hapo.
NGOMA VS SOLIA
Mafundi wengine ambao kama watapangwa wataonyeshana ubabe zaidi ni Fabrice Ngoma anayecheza eneo la kiungo wa kati Simba sanbamba na Amr El Solia anayecheza eneo hilo pia.
Wawili hawa wote ni wakali kwenye kukaba, kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi hivyo itakuwa burudani kuwatazama.
KANOUTE VS RABIA
Kiungo Sadio Kanoute kwa sasa pale Simba kuna mechi anatumika kama namba 10, pale wanapoanza sambamba na Sarr na Ngoma na amekuwa akifanya vizuri ikiwemo kufunga.
Kama itakuwa hivyo basi atakutana na kazi kutoka kwa mkali ambaye mara kadhaa hucheza eneo la beki wa kati, Rami Rabia. Wakali hawa watakuwa na bato ya kila mmoja kulitetea chama lake na atakayeshinda hapa basi atakuwa mwamba zaidi.
CHAMA VS TAWFIK
Mkali huyu wa Simba, Clatous Chama ndiye injini ya Simba husasani kwenye mechi za kimataifa ambapo hucheza kama mshambuliaji anayetokea kushoto.
Kwenye gemu hii atakutana na beki kitasa Akram Tawfik ambaye pia amekuwa na kiwango bora. Hii itakuwa vita ya kifundi kwani wote mguuni umo.
SAIDO VS MAALOUL
Saindi Ntibanzokiza ni nguzo ya Simba lakini hapa atakutana na beki mzoefu Al Maaloul ambaye pia ni nguzo ya Ahly kwenye kukaba na kuanzisha mashambulizi.
Hii itakuwa bato ya wakongwe kazini kwani Saido ana miaka 36, huku Maaloul akiwa na 34.
JOBE VS ABDELMONEM
Straika Mgambia Pa Omar Jobe ndiye amekuwa akipewa nafasi kwenye mechi ngumu za CAF na hapa kama atapangwa basi atakutana na beki katili Mohamed Abdelmonen ambaye ni chaguo la kwanza kikosini Al Ahly.
Hii itakuwa bato ya heshima kwani Jobe atataka kufunga wakati Abbdelmonem atakuwa anataka kuonyesha kuwa yeye ni kisiki cha mpingo. Tusubiri tuone.
BENCHIKHA VS KOLLER
Hii itakuwa vita ya Mswiss Marcel Koller na Mualgeria Abdelhak Benchikha wa Simba.
Hapa Benchikha anafaida ya uzoefu kwani analijua vyema soka la Afrika kuliko Koller ambaye Ahly ni timu yake ya kwanza kufundisha ukanda huu.
Wawili hawa ndio wataamua mechi kutokana na mbinu, ufundi na wachezaji watakaoamua kuwatumia kwenye mechi hizo mbili.