Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, APR zaibeba Afrika Mashariki

Bff144fd64423d206adff9ca6b088978 Simba, APR zaibeba Afrika Mashariki

Tue, 1 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SIMBA ya Tanzania Bara na APR ya Rwanda ndizo timu pekee za ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilizoshinda mechi zao za mwanzo za Ligi ya Mabigwa Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wakati Simba na APR zikishinda, timu zingine za ukanda huo, Gor Mahia ya Kenya, Vipers ya Uganda na Mlandege ya Zanzibar zimejiweka katika nafasi ngumu baada ya kufungwa katika mechi zao.

Simba walianza vizuri licha ya kucheza ugenini baada ya kuifunga Plateau ya Nigeria katika mchezo uliofanyika nchini humo, huku bao pekee katika mchezo huo likifungwa na Clatous Chama baada ya kupata usaidizi kutoka kwa Luis Miquisone katika dakika ya 58.

Wawakilishi hao wa Tanzania ambao wanatarajiwa kurejea nchini leo kutoka Nigeria, endapo watapata ushindi wa jumla na kuvuka hatua hiyo ya awali, watacheza na mshindi wa jumla kati ya Costa do Sol ya Msumbiji na RC Platinum ya Zimbabwe. Katika mchezo wa kwanza, Platinum ilishinda 2-1.

APR walifanya kweli dhidi ya klabu nyingine ya nchi ya Afrika Mashariki ya Gor Mahia ya Kenya baada ya kuichapa 2-1 katika mchezo uliofanyika Kigali kwenye Uwanja wa Amahoro.

Timu hiyo ya Rwanda inayomilikiwa na jeshi ilitawala mchezo huo na dakika tisa tangu kuanza kwa mchezo, ilipata bao kupitia kwa kiungo wake, Olivier Niyonzima baada ya mpira wa adhabu uliopigwa vizuri na Djabel Manishimwe.

Hatahivyo, wageni Gor Mahia walisawazisha katika dakika ya 27 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Keneth Muguna baada ya makosa ya kipa wa APR, Omar Rwabugiri.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1, huku APR ikilisakama zaidi lango la wapinzani wao na kusababisha Gor Mahia kujifunga kwa bao la Fitina Ombolenga katika kipindi cha pili.

Kwa upande wa Uganda, wawakillishi wao Vipers walijikuta wakianza vibaya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa 1-0 na Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo uliofanyika Kampala.

Waleed Bakhiet ndiye alikuwa shujaa baada ya kuwapatia bao la ushindi wageni Al Hilal katika dakika ya 25, akitumia vizuri makosha ya mabeki ambao walishindwa kuzuia mpira mrefu wa kurushwa kutoka upande wa kulia.

Nayo timu ya Mlandege ya Zanzibar ilijikuta ikikiona cha mtema kuni baada ya kupokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa CS Sfaxien ya Tunisia katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani humo.

Wawakilishi wa Burundi katika michuano hiyo, Le Messager ambao walitakiwa kucheza ugenini dhidi ya Young Buffalos FC ya eSwatini juzi , mchezo wao uliahirishwa na ulitarajia kuchezwa jana baada ya timu hiyo ya Burundi kukosa ndege.

Chanzo: habarileo.co.tz