Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City wameendelea kumshinikiza Bernardo Silva asaini mkataba mpya katika klabu hiyo na kuzima uvumi wa uhamisho unaomzunguka nyota huyo wa Ureno, kwa mujibu wa ripoti.
Silva amekuwa na uvumi mkubwa wa kuondoka Man City kipindi hiki cha usajili wa kiangazi baada ya kubeba makombe matatu msimu uliopita.
Hata hivyo, City wanatamani mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aongeze mkataba mpya wa kuendelea kubaki jijini Manchester.
Silva amebakiza mkataba wa miaka miwili aidha Man City inataka kumwongeza mkataba mwingine wa miaka miwili kwa mujibu wa ripoti.
Mkataba huo mpya utaongeza mshahara wake na kufikia Pauni 300,000 kwa wiki na kwa mujibu wa gazeti la Mirror, Man City wanamshinikiza kiungo huyo ajibu maboresho hayo na kufuta uvumi huo.
Barcelona ndio timu inayovutiwa na kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno kwa muda mrefu, huku Rais wa klabu hiyo Joan Laporta, akikiri anatamani amsajili.
Aidha Paris Saint-Germain imekuwa ikiwasiliana na Man City ili itoe ofa na kubadilishana wachezaji kama sehemu ya uhamisho wa Silva.
Iwapo Silva atafanya uamuzi wa kuachana na mabingwa hao wa Ligi Kuu England, klabu hiyo ina nia ya kutafuta mbadala wake na tayari wamehusishwa na kutaka kumnunua kiungo wa Inter, Nicolo Barella.
Silva tayari amejiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na hakuna tatizo lolote na mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno, huku Pep Guardiola akifurahishwa na uwamuzi wake aliporejea.