Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sillah humwambii kitu kwa wali mandondo

Sillah Raja Gibril Sillah.

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miundombinu ya Azam FC kwa mara ya kwanza ilimshangaza mshambuliaji wake wa kimataifa, Gibril Sillah kabla hajaonja kucheza mechi za mikoani ambako nako alijifunza somo lake.

Mahojiano maalumy yaliyofanywa baina ya Mwanaspoti na Sillah, anaeleza kitu kilichomshangaza baada ya kutembezwa kwenye miundo mbinu ya Azam hakuona kama Tanzania ipo tofauti na Morocco alikokuwa ametoka.

Anasimulia “Nilishangazwa sana kuona namna ambavyo Azam imejiwekeza kwenye miundo mbinu, sikutegemea kukuta wana uwanja na kila kitu kinachotakiwa kwenye soka, sikuona tofauti kubwa na Morocco nilikokuwa nimetoka,” anasema na kuongeza;

“Sasa nikaja kujua utofauti baada ya kwenda mkoani kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, nikaona miundombinu ipo tofauti na ya Azam FC nikaendelea kujifunza zaidi namna ya kujipanga ili kuweza kucheza kwa kiwango kikubwa.”

Ukiachana na kushangazwa na miundombinu ya Dodoma, lakini mechi hiyo ni kati alizotaja zimeingia kwenye rekodi za maisha yake, hatazisahau kutokana na kukutana na mabeki wanaotumia mabavu sana.

“Mebeki wanatumia nguvu na nisingekuwa makini ni rahisi kuumia, kuna wakati unawaza kama unakamiwa, lakini ikanifunza kuuelewa mpira wa Tanzania,”anasema.

ALIVYOTARAJIWA

Sillah ambaye kabla ya kujiunga na Azam FC aliichezea miamba ya soka la Morocco, Raja Casablanca, anasema ni kawaida kwa mashabiki kutaka kuona wachezaji wao wapya wakionyesha thamani zao ndani ya kipindi kifupi.

“Binafsi sina presha yoyote kwa sababu najua hii ni ligi na nchi tofauti kabisa na kule nilikotoka, kuna vitu huwa vinakuja tu vyenyewe, nimejitahidi kuwasoma wenzangu ili kwa pamoja tufanikishe malengo ya timu,” anasema na kuongeza;

“Naamini ndani ya kipindi kifupi kila kitu kitakuwa sawa, nimekuwa mchezaji mwenye kupenda mafanikio na mwenye mtazamo chanya siku zote, tusubiri muda utaongea.”

SIMBA/ YANGA KIMATAIFA

Kabla hajasajiliwa Azam akiwa na Raja Casablanca ya Morocco, ilikuwa ikitajwa Tanzania wachezaji wengi walikuwa wanatamani kupata nafasi ya kuitumikia Simba kutokana na ushiriki wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).

“Wachezaji wa mataifa mengi walikuwa wanaitazama Simba, kutokana na kufika hatua ya robo fainali mara nyingi, hiyo ilifanya baadhi ya mastaa kufuatiliwa kwa ukaribu.

“Ndio maana ilikuwa rahisi kuwajua kina Clatous Chama, Luis Miquissone ambao walifanya vizuri kwenye michuano hiyo, ukiondoa rafiki yangu Pape Sakho.”

Mbali na Simba aliitaja Yanga kuanza kufanya vizuri kimataifa, baada ya mwaka jana kufika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kwa sasa Yanga inaingia kwenye anga za Simba ambayo tayari ilijiwekea mizizi yake kwenye michuano ya CAF hilo linaonyesha namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kubwa ya kukua kwa soka,” anasema.

MASTAA HAWA

Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita, Fiston Mayele ambaye kwa sasa anaichezea Pyramids ya Misri na kiungo fundi wa Simba, Chama ni miongoni mwa wachezaji ambao Sillah alikuwa akivutiwa nao kabla ya kujiunga na Azam FC.

“Nilikuwa nikiongea na Sakho kabla ya kufanya maamuzi ya kujiunga na Azam, wakati nikifuatilia ligi ya Tanzania niliona wachezaji ambao uwezo wao nikavutiwa nao kama Mayele, Chama, Henock Inonga.

“Uwezo wao ni mkubwa na ni watu poa sana ambao naamini tutaendelea kuipa thamani ligi ya Tanzania.”

KWA NINI AZAM?

Nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili na hata nyuma ya mshambuliaji wa kati, namba 10, anasema sababu iliyomsukuma kujiunga na Azam FC ni mipango waliyonayo.

“Nilikuwa na ofa ya kwenda Ufaransa lakini nikaona bado nina nafasi ya kufanya kitu sehemu nyingine kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Afrika, Azam ina mipango mingi mizuri ambayo naamini tunaweza kuifanikisha,” anasema.

Hata hivyo, baada ya kujiunga na Azam, anakiri kuona ushindani wa namba kutokana na aina ya wachezaji ambao amewakuta kwenye kikosi hicho ambacho kipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Simba ikiwa na pointi 13.

“Nimekuwa nikipenda changamoto, kiukweli Azam ina wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo mkubwa kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kuwa moja ya timu tishio sio kwa Tanzania tu hata Afrika,” anasema.

MAISHA YA BONGO

Kwanza kabisa anafurahia vyakula na anachopendelea zaidi wali na maharage, ingawa si chakula cha asili ya kwao.

“Nilipoonja kwa mara ya kwanza nilipenda sana, kiukweli Watanzania wanajua kupika, unakula unasikia ladha nzuri ya chakula halisi.”

Ukiachana na chakula, anazungumzia Tanzania ina watu wakarimu ambao wanamfanya asijisikie mgeni, ingawa changamoto kubwa inayomkabili ni Kiswahili, kwani kuna wakati anatamani kufanya vitu ila anashindwa namna ya kuwasiliana nao.

“Napenda kujifunza Kiswahili, ili kinarahisishie kuzungumza na watu na kufanya baadhi ya shughuli zangu, kwa sasa najua mambo na kuitikia poa na shwari, aliyenifundisha ni Idris Mbombo na ndiye muda mwingi ananisemesha,” anasema.

Kitu kingine kilichomshangaza kwenye mtandao wake wa kijamii (instagram) baada ya kusaini Azam FC alishangazwa kuona amepata wafuasi wengi, huku baadhi wakienda mbali zaidi kwa kumuandikia ujumbe wa ndani yaani (DM).

“Wapo wanaopenda ninavyocheza, wengine wanaomba urafiki kawaida, wanaonipa moyo wa kujituma ili niifanyie makubwa klabu yao, hivyo yote nayachukua kama changamoto ya kuongeza bidii kwenye kazi zangu,” anasema.

KANUFAIKA NA SOKA

Sillah ambaye anapenda sana kucheza video gemu, anasema soka limebadilisha maisha yake kwa ujumla, kama ilivyo ndoto za wengi kumiliki nyumba zao, hilo kwake limetimia.

“Nimejenga kwetu, naisaidia familia yangu kupitia soka, siwezi kusema nimefikia kila kitu kwenye ndoto zangu, nimeyafanikisha baadhi mengine naendelea kupambana ipo siku nitaishi ndoto zangu,” anasema Sillah ambaye nje na soka fani yake ni benka na pia anaupenda mchezo wa kikapu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live