Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ametatua mgogoro wa muda mrefu wa kugombea ubia walioingia kati ya Sauli Henry Amon na familia ya mzee Bushiri Pazi katika jengo la ghorofa nane lililopo Kariakoo, Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.
Amon ni Mbunge wa zamani wa Rungwe, aliingia kwenye mgogoro huo wa jengo la ghorofa nane lililoko Kariakoo jijini hapa, baada ya Mahakama ya Rufani kueleza kuwa nyumba hiyo ilijengwa kwenye kiwanja kilichouzwa kwa mnada isivyo halali.
Jengo hilo ni nyumba namba 113, kitalu namba 4 block namba 17, lenye ghorofa nane lililopo Kariakoo, Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam
Amon, aliyekuwa mbunge kupitia CCM mwaka 2015 -2020 anayejulikana zaidi kwa jina la biashara la S.H. Amon, anamiliki kampuni ya S.H. Amon Enterprises Co. Ltd yenye maduka ya vipodozi jijini Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Amon aliinunua nyumba hiyo ya kawaida kwenye mnada Mei 13, 2001 kwa Sh 105 milioni kupitia Kampuni ya S.H. Amon Enterprises Co. Ltd na kupewa hati namba 57275 iliyotolewa Machi 24, 2005, kwa jina la kampuni hiyo, kabla ya kuibomoa na kuporomosha ghorofa hilo.
Awali kiwanja hicho kilikuwa na nyumba ya udongo ambayo iliuzwa baada ya familia ya watoto sita ya marehemu Pazi kupata fursa wakaingia ubia na mwekezaji (hakutajwa) aliyeivunja na kujenga nyumba nyingine ya kisasa kwa makubaliano ya kibiashara.