Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku ya Waafrika; Morroco, Ufaransa mziki wote unapigwa hivi

Morocco Pic Dataaaaaaa.png Morocco ina nafasi ya kuandika historia kwa Bara la Afrika

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ufaransa imepiga hatua muhimu katika kuelekea kitu adimu - kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia baada ya kuichapa England Jumamosi iliyopita. Na sasa watakipiga na Morocco kwenye nusu fainali itakayopigwa leo Jumatano, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ikishinda mechi hiyo, Les Bleus itakuwa imebakiza ushindi mmoja tu kuwa nchi ya kwanza tangu Brazil ilipotetea taji la ubingwa wa Kombe la Dunia 1962.

Lakini, waliosimama mbele yao ni Morocco yenye mzuka mkubwa, ikiwa taifa la kwanza kutoka Afrika kufikia nne bora kwenye fainali za Kombe la Dunia, huku kwenye fainali hizo za Qatar imeruhusu bao moja tu kwenye nyavu zao na imezitupa nje Hispania na Ureno na kuthibitisha tu kwamba wao siyo wa kuwachukulia kawaida.

Na hata bao lenyewe walilofungwa ni lile walilojifunga wenyewe kwenye mechi dhidi ya Canada. Hispania walishindwa kugusa nyavu za Morocco hata ulipofikia wakati wa kupigiana penalti na miamba hiyo ya La Roja, ilipiga mikwaju mitatu.

Lakini, kinachoulizwa kwa sasa makocha Didier Deschamps na Walid Regragui watatoka na mtoko gani kwenye kipute hicho kitakachopigwa uwanjani Al Bayt? Mambo ni moto.

Kwa upande wa Ufaransa, kocha Deschamps hatarajiwi kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake cha kwanza kilichoanza kwenye mchezo wa robo fainali na kuwachapa England mabao 2-1.

Hiyo ina maana, nahodha Hugo Lloris, moja ya mastaa wa maana kabisa waliofanya kweli dhidi ya England ataendelea kusimama golini kwenye mchezo huo ambao utakuwa wa 144 kwake kuitumikia Les Bleus.

Mbele yake kutakuwa na ukuta wa wakali wanne Jules Kounde, Raphael Varane, Dayot Upamecano na Theo Hernandez. Beki Upamecano alikosolewa sana kwa kiwango chake, hasa kwa namna alivyokuwa akipata shida kumzuia straika Harry Kane, hivyo Deschamps kama atahitaji kumbadilisha anaweza kuanza na ama Ibrahima Konate au William Saliba.

Hernandez, ameziba vyema pengo la kaka yake Lucas - aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Australia, kwenye mechi ya England alikuwa na bahati hakutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mason Mount iliyosababisha penalti ambayo Kane alikosa.

Huko Ufaransa, mechi zake zote ilizocheza imeruhusu mpira kutinga kwenye nyavu zao, hivyo kocha Deschamps atakuwa anapiga sana sala za kuhakikisha timu yake inafunga mabao mengi kuliko wapinzani wao ili kushinda mechi.

Kwenye sehemu ya kiungo, Aurelien Tchouameni na Adrien Rabiot wameendelea kutengeneza kombinesheni bora kabisa, wakitengeneza msingi wa kuwafanya mastaa wanne wanaosimama mbele yao kupanga vyema mashambulizi.

Safu yao ya ushambuliaji itaongozwa na Olivier Giroud huku Ousmane Dembele akiwa upande wa kulia, Kylian Mbappe kushoto na Antoine Griezmann akifanya mambo yake kwenye Namba 10.

Kingsley Coman ni mchezaji pekee aliyeingizwa kwenye mechi ya Jumamosi, bila ya shaka ataendelea kusubiri benchi pia hata kwenye mechi hiyo ya nusu fainali dhidi ya wagumu Morocco.

Kwa upande wa Morocco, wao kikosi chao kimeandamwa na majeruhi, wagonjwa na wengine wanatumikia adhabu ya kadi.

Noussair Mazraoui na Nayef Aguerd walikosa mchezo wa robo fainali dhidi ya Ureno, wakati Romain Saiss alitolewa kwa machera katika mchezo huo dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza.

Mazraoui na Aguerd wanaweza kuwa fiti na kurejea mzigoni kwenye kipute hicho cha leo - licha ya wakali waliocheza badala yao kwenye mechi ya Ureno, Yahia Attiyat Allah na Jawad El Yamiq nao walifanya vyema kuwadhibiti Ureno.

Walid Cheddira, hatakuwapo kwenye mchezo huo wa nusu fainali baada ya kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa njano mbili kwenye mchezo. Atakuwa na adhabu ya mechi moja, hivyo Morocco ikitinga fainali atatumika fainali.

Hivyo kocha Regragui ataendelea kuwa na chaguo la Yassine Bounou golini ambaye atalindwa na mabeki wanne Achraf Hakimi, El Yamiq, Aguerd na Allah.

Kwenye sehemu ya kiungo kutakuwa na wakali watatu Azzedine Ounahi, Sofyan Amrabat na Selim Amallah ambao wamekuwa wakipiga kazi kubwa kuwafanya wakali wao watatu kwenye eneo la kushambulia Hakim Ziyech na Sofiane Boufal wanaocheza pembeni kumchezesha vyema straika wao Youssef En-Nesyri - aliyepiga bao lililowazamisha Ureno Jumamosi.

Macho na masikio ya wengi yanasubiri kuona ni kikosi gani kitapenya kwenye mchezo huo, huku fainali itapigwa Jumapili.

Rekodi zinaonyesha Morocco na Ufaransa zimekutana mara mbili tu, zote kwenye mechi za kirafiki. Zilipokutana mara ya mwisho ilikuwa 2007 - ambapo mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku mechi ile ya kwanza iliyopigwa mwaka 2000, Ufaransa iliangusha kipigo cha mabao 5-1 kwa Morocco. Kwenye mchezo huu wa mashindano, nani atatoboa?

Chanzo: Mwanaspoti