Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku tano moto Yanga, Simba

Said Hersi 1140x640 Rais wa Yanga, Hersi Said

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Itakapofika Jumapili Januari 15, saa 00:00 usiku dirisha dogo la usajili litafungwa rasmi kwa klabu zote za Ligi Kuu Bara na hata ligi za chini lakini wakati zimesalia hizo kuna moto mkubwa kwa klabu kongwe Simba na Yanga katika kusajili watu wa maana wanaowataka.

Usajili ambao unazigonganisha vichwa klabu hizo mbili ni juu ya kuboresha safu zao za ushambuliaji na zote zikihitaji wachana nyavu wenye makali zaidi.

Yanga inataka kuingiza mshambuliaji mmoja anayejua kufunga na tayari Mwanaspoti linafahamu mabosi wa klabu hiyo wako katika hatua za mwisho kabisa kumtambulisha Mzambia Kennedy Musonda, watakayemsajili kutokea Power Dynamos ya nchini kwao.

Yanga imeshamalizana na Musonda kila kitu kilichobaki ni utambulisho tu wanaoendelea kuupanga lakini mtihani wao kwao ni kwamba atachukua nafasi ya nani kutokana na klabu hiyo kuwa na wachezaji 12 wa kigeni.

Yanga inafikiria kuwatema wachezaji wawili wa kwanza ni Heritier Makambo ambaye yuko katika hatua za mwisho kuachwa lakini sambamba na Musonda anayetakiwa kuingia, Yanga pia ilikuwa inafikiria kumrudisha kundini Yacouba Sogne ingawa usajili wake unaonekana kuingia mchanga.

Mabosi wa Yanga wanaona Yacouba hajawaridhisha kuingia katika kikosi hicho akihitaji muda zaidi wa kutafuta ufiti ingawa mapema mabosi wa benchi la ufundi nao wakiona jamaa anaweza kurejea katika usajili wa kikosi hicho ili apewe mechi za kuanza kucheza taratibu.

Wakati huohuo Yanga pia inapiga hesabu za kutaka kusajili beki wa kati ambapo usajili huo unawezekana kukwama kama utata wa Yacouba hautamalizika kwa haraka ndani ya siku tano zilizobaki.

Winga wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila akizungumzia hatma ya Yacouba alisema kwa kiwango ambacho amekionyesha raia huyo wa Burkina Faso bado hajaonyesha kuwa tayari kumshawishi kuingia kikosi hicho katika dirisha hili la usajili.

"Tumemuona Yacouba katika hizi mechi mbili za Kombe la Mapinduzi kwa mtazamo wangu naona bado hajawa katika kiwango bora cha kuhitaji kumuingiza dirisha hili, unajua mara nyingi dirisha kama hili unahitaji kumuingiza mtu ambaye yuko tayari ana moto ambaye anakuja kuendeleza na sio kuja kutafuta kasi akitokea chini, tuwaachie makocha nao watakuwa na maoni yao katika hilo," alisema Lunyamila.

Tayari Yanga imeshaibuka kwa kumtambulisha staa mmoja mzawa hadi sasa kiungo wa kati Mudathir Yahya aliyeanza kuitumikia klabu hiyo Kombe la Mapinduzi akionekana anaweza kufiti.

Wakati Yanga wakipasua vichwa hivyo, Simba nako kuna vita kama hiyo wakiwa Dubai walikoweka kambi ya muda mfupi tayari kocha wao mpya Mbrazil Roberto Olivieira 'Robertinho' amethibitisha akiwaambia mabosi wake kwamba anahitaji mshambuliaji wa kati haraka.

Baada ya kuwaona wachezaji wake wote katika mazoezi ya siku mbili tu yametosha kwa Robertinho kuonyesha kwamba anatamani kuwa na mshambuliaji mwingine wa mwisho kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Simba hadi sasa imeshamuingiza kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ambaye tayari katika mchezo wake mmoja tu umetosha kuifungia timu hiyo mabao matatu 'hat trick' dhidi ya Prisons.

Simba ilishafanya majaribio mawili ya kusaka washambuliaji Mkongomani Cesar Manzoki ambaye bado klabu yake ya China imeendelea kumbakiza huku Kwame Opoku ambaye naye usajili wake uliingia mdudu kufuatia kuumia hivi karibuni sasa wana kazi ndani ya siku hizi zilizobaki kumridhisha kocha wao kwa kuleta mshambuliaji na ni lazima waachane na mgeni mmoja, huku mkongwe Mundele Makusu wa FC Lupopo akitajwa pia kuwa anaweza kutua Msimbazi.

Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes ameliambia Mwanaspoti kuwa anakubaliana na mtazamo wa Robertinho, akisema usajili wa mshambuliaji huyo mpya utaongeza nguvu zaidi ya kikosi hicho kwenye mashindano ya Kimataifa.

"Simba inahitaji watu kama watatu ninavyoona mimi lazima wasajili viungo wawili, mmoja awe mchezeshaji na mkabaji lakini pia watafute mshambuliaji, kama kocha kasema anataka mshambuliaji mimi binafsi naungana naye," alisema Nemes.

"Ukiangalia kwa mashindano ya ndani huwezi kuona kama kwa sasa Simba inahitaji mshambuliaji lakini ukizitazama mechi zijazo za kimataifa utaona kuna haja ya kutafuta mshambuliaji mwenye makali."

Chanzo: Mwanaspoti