Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku saba ngumu kwa Benchikha

Benchikha Morocco.jpeg Kocha Benchikha

Fri, 22 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameiangalia ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara kwa timu hiyo ya kufungia mwaka 2023 na kukiri ni ngumu kwelikweli, lakini akatoa kauli ya kibabe kwamba anakipanga kikosi hicho ili kuhakikisha kinatoboa na kuiweka timu katika nafasi nzuri ikiingia Mwaka Mpya wa 2024.

Benchikha aliyeanza kuwapa raha mashabiki na wapenzi wa Simba kutokana na matokeo mazuri inayopata timu hiyo na kuupiga mpira mwingi tangu akabidhiwe kikosi kutoka kwa Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye alitimuliwa mara baada ya Simba kuchapwa mabao 5-1 na Yanga, ana siku saba za kuonyesha umwamba.

Simba inakabiliwa na michezo mitatu ya Ligi Kuu ndani ya siku saba kabla ya mwaka huu kumalizika, akianza na kesho kuikabili KMC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Kino Boys wakiwa ndio wenyeji, kisha itasafiri hadi Kigoma kuvaana na Mashujaa Desemba 26 na kabla ya Desemba 29 kucheza na Tabora United.

Hii ikiwa na maana itakuwa na mapumziko ya siku mbili kabla ya kucheza mchezo mmoja, kitu ambacho kocha huyo kutoka Algeria alisema ni mtihani mzito kwa wachezaji, lakini hakuna namna zaidi ya kujipanga na kupata matokeo mazuri yatakayowaweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi unaoongozwa kwa sasa na Azam FC.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Benchikha alisema kadri ambavyo anazidi kukaa na wachezaji, ndivyo wanavyoelewa mbinu zake huku akiwataka kuendelea kupambana katika michezo iliyobakia licha ya ratiba yao kubana.

“Tuna siku ngumu na muhimu kwetu kabla ya kumaliza mwaka huu, lakini hatuna kisingizio zaidi ya kucheza kwa ajili ya timu na kupata matokeo bora yatakayotusaidia kuendelea kurejesha morali ya wachezaji kikosini na mashabiki wetu kwa ujumla ambao wamekuwa wanatuunga mkono,” alisema Benchikha.

Wakati Benchikha akizungumza hivyo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba katika siku hizo saba ndizo ambazo kocha huyo atazitumia kufanya uamuzi wa mwisho kwa wachezaji ambao watapewa mkono wa kwaheri kwenye dirisha hili la usajili.

Chanzo makini kutoka ndani ya Simba, kinasema viongozi wa klabu hiyo tayari wamekuwa na vikao na Benchikha kwa ajili ya kujadili kuhusu maingizo mapya na watakaoondolewa, ingawa bado muafaka wa mwisho haujafikiwa huku panga likiwahusu zaidi wale ambao wamekuwa hawana nafasi.

“Anataka kuzitumia mechi hizo za funga mwaka kukusanya pointi, lakini kuwasoma kwa mara ya mwisho wachezaji kabla ya kupitisha panga kwa wale ambao angependa watolewe kikosini na kuruhusu wapya kuingia, kwani muda uliosalia ni mchache kabla ya dirisha kufungwa Januari 15,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.

Benchikha aliyetangazwa rasmi kukiongoza kikosi cha Simba Novemba 24 baada ya kutemwa kwa Robertinho, ameisimamia katika mechi nne hadi sasa.

Mechi hizo tatu ni za Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ikishinda moja, sare moja na kupoteza pia moja, huku katika Ligi Kuu akiiongoza katika mechi moja ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambayo Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa kujiamini wa mabao 3-0.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live