Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 9 za moto Simba na Yanga

Simbaa Yanga Pic Siku 9 Siku 9 za moto Simba na Yanga

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: dar24.com

Klabu za Simba na Yanga zina siku 9 za moto kuanzia leo za kuhakikisha zinachanga karata zake vizuri wakati zitakapokuwa zinakabiliana na ratiba ya Ligi Kuu Bara, michuano ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho Afrika.

Katika kipindi hicho Simba inakabiliwa na michezo mitatu ambapo miwili itakuwa ya kimashindano na mmoja wa kirafiki wakati vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga itacheza mechi mbili tu na zote zitakuwa ni za mashindano.

Simba itaanza kuchanga karata zake kwa kucheza na Singida Big Stars keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mchezo wa pili wa marudiano baada ya awali timu hizo kufungana bao 1-1 Novemba 9, mwaka jana kwenye Uwanja wa Liti.

Siku moja baada ya mchezo huo Simba itashuka tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 5, kucheza mechi ya kirafiki na Al Hilal ya Sudan inayojiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini. Baada ya hapo itaanza rasmi kampeni zake katika Ligi ya

Mabingwa hatua ya makundi kwa kusafiri kupambana na Horoya ya Guinea, Februari 11, mchezo ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa General Lansana Conte uliopo mji mkuu Conakry.

Mchezo huo unavuta zaidi hisia za mashabiki wengi wa soka kutokana na viwango vya timu zote mbili katika mashindano ya ndani ambapo Simba katika michezo 21, iliyocheza imeshinda 15, sare mitano na kupoteza mmoja ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya mabingwa watetezi Yanga iliyopo kileleni na pointi zake 56.

Horoya inaongoza Ligi ambapo katika michezo 13 iliyocheza imeshinda tisa, sare miwili na kupoteza miwili ikiwa na pointi 29, huku eneo la ushambuliaji likiwa tishio kufuatia kufunga mabao 20 na kuruhusu manne tu.

Kwa upande wa Yanga itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi hii kucheza na Namungo huku ikiwa na rekodi zuri ya kushinda mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Majaliwa Desemba 7, mwaka jana kwa kuifunga mabao 2-0.

Timu hizi zinakutana huku Yanga ikiwa na rekodi zuri dhidi ya wapinzani wake kwani tangu Namungo imepanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020, haijawahi kushinda, ikifungwa mara mbili huku michezo mitano ikiisha kwa sare.

Baada ya hapo itasafiri hadi Tunisia kucheza na Monastir katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa Februari 12,ikiwa na kumbukumbu nzuri mara ya mwisho ilipotembelea huko kufuatia kuitoa Club Africain.

Mchezo huo hautokuwa rahisi kwa Yanga kwani hata wapinzani wao katika Ligi ya Tunisia wanafanya vizuri pia kwani inaongoza kundi B na pointi zake 25 baada ya kucheza michezo 11 ikishinda nane, sare mmoja na kupoteza miwili.

Akizungumzia ratiba hiyo nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kikubwa kinachotakiwa kwa miamba hiyo ni kujipanga vizuri hasa kwenye michuano ya kimataifa ambayo timu zote mbili zinaazia zikiwa ugenini.

"Ukiangalia ratiba ni ngumu kwa siku zilizobaki hususani kucheza ugenini ambapo itawabidi waanze taratibu za safari mapema lakini niseme tu hizi timu zina watu weledi ambao naamini mipango yote wameshaiweka vizuri."

Nyota wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila alisema kwa ubora wa timu zote mbili kwa sasa bado anaona zina nafasi ya kufanya vizuri licha ya kuwataka kujiandaa vyema kwani wapinzani wao watataka kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

Chanzo: dar24.com