Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 53 za moto Yanga

28281 Yanga+pic TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Yanga inapitia kipindi kigumu kwa sasa, lakini wiki saba zijazo zitakuwa moto zaidi kwa klabu hiyo kwa kuwa ndizo zitaamua kuipa neema au kilio katika msimu huu unaoendelea.

Mchakato wa uchaguzi mkuu unaoendelea, kipindi cha dirisha dogo la usajili na hali ngumu ya kiuchumi ambayo inaisumbua Yanga kwa sasa, ni mambo matatu makubwa na yenye uzito wa kipekee ambayo klabu hiyo itakumbana nayo ndani ya kipindi hicho cha siku 53.

Miongoni mwa changamoto hizo tatu ambazo Yanga itazipitia, kubwa zaidi ni mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ambao unatarajiwa kufanyika Januari 13, mwakani kwa mujibu wa utaratibu na muongozo uliotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayosimamia uchaguzi huo.

Katika kipindi chote kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi, wanachama na mashabiki wa Yanga watakuwa wanaumiza kichwa kujua ni viongozi gani hasa miongoni mwa waliotangaza nia watakuwa na uwezo wa kuirudisha timu yao kwenye mstari.

Taswira ya maisha ambayo klabu hiyo ilipitia pindi ilipokuwa ikiongozwa na mfanyabiashara bilionea, Yusuf Manji akiwa mwenyekiti na mfadhili wa klabu hiyo, bila shaka itawaweka kwenye wakati mgumu wagombea waliochukua fomu za kuwania uongozi hasa wale wanne waliojitosa kutaka ridhaa ya wanachama Januari 13.

Ndani ya kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi, wagombea Dk Jonas Tiboroha, Mbaraka Igangula, Yono Kevela na Erick Ninga watakuwa kwenye presha kubwa ya kuwaaminisha Wanayanga ambao wengi wameonyesha kutofurahishwa na maisha ambayo timu yao inapitia kama watakuwa na uwezo wa kuirudisha kwenye ufalme wa zamani na kupambana vilivyo na Simba, Azam FC zinazoonekana tishio kwao.

Tangu Manji alipoandika barua ya kujiuzulu na kuanza kujiweka pembeni ndani ya klabu hiyo, hadi sasa viatu vyake vimeonekana kuwa vigumu kuvalika ndani ya Yanga, hivyo ni mtihani mkubwa kwa wagombea na wanachama wa klabu hiyo kupima nani mtu sahihi wa kuwarudisha pale walipokuwa.

Lakini wakati suala la uchaguzi likipamba moto, Yanga inakabiliwa na usajili wa dirisha dogo ambapo inapaswa kuimarisha kikosi chake kwa kuwatoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji na kuleta wapya.

Kwa bahati mbaya hilo linatokea katika kipindi ambacho Yanga inakabiliwa na ukata jambo ambalo linaweza kuifanya ishindwe kupata aina ya wachezaji ambao benchi la ufundi linaamini kuwa wataifanya timu hiyo kuwa tishio.

Ukosefu huo wa fedha mbali na kuifanya Yanga ipate wakati mgumu wakati huu wa kipindi cha dirisha dogo la usajili, unaweza pia kuathiri mwenendo wake kwenye ligi kutokana na migomo ya mara kwa mara ya wachezaji inayotokana na kutolipwa sehemu ya fedha za usajili, mishahara na posho.

Changamoto ya fedha inavyoathiri mipango ya Yanga kwenye dirisha la usajili na mwenendo kwenye ligi, imethibitishwa na Kocha Mkuu Mwinyi Zahera aliyedai kuwa nyota wake wawili nahodha Kelvin Yondani na Beno Kakolanya wamegoma kusafiri na timu kwenda Shinyanga kwa sababu ya madai.

Akizungumza kwa simu jana, Zahera alisema ana dhamira ya kusajili wachezaji wapya, lakini anashindwa kwa sababu klabu haina fedha.

“ Nimefika hapa Mwanza lakini wachezaji Kelvin Yondani na Beno Kakolanya hawapo kwa sababu ya madai yao. Nataka kusajili lakini kumpata mchezaji mpya inatakiwa fedha nyingi. Itakuwa vigumu kumnunua mchezaji halafu baadaye unamkopa,” alisema Zahera.

Wingu zito lililotanda Yanga, limewaibua nyota wa zamani wa timu hiyo, Abeid Mziba na Ally Mayay kwa nyakati tofauti walitoa maoni.

“Ninashauri bodi ya wadhamini na viongozi waliopo wakutane waunde kamati ya kutafuta fedha ili kupunguza ukali wa ukata klabuni,” alisema Mayay.

Mziba alipongeza ujasiri wa Zahera kwa kuwa mkweli na ametoa rai kwa viongozi wa Yanga kuchukua tahadhari mapema kuwanusuru wachezaji na mazingira magumu ya kutekeleza majukumu yao hasa kipindi hiki cha usajili.



Chanzo: mwananchi.co.tz