Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 373 za Mnyama zilivyogeuka mateso kwa Mkapa

Tano Ta Yanga Siku 373 za Mnyama zilivyogeuka mateso kwa Mkapa

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Acha na kipigo cha mabao 5-1 ilichopewa Simba juzi na watani wao wa jadi, Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara, matokeo hayo yamehitimisha ubabe wa Mnyama wa siku 373 kucheza bila kupoteza kwenye ligi hiyo, ikiwa imecheza jumla ya mechi 28 mfululizo.

Simba ilikumbana na kipigo hicho kikubwa cha kwanza kwa timu hiyo mbele ya watani, tangu iliponyukwa mabao 5-0 katika mechi ya Kariakoo Derby iliyopigwa Juni Mosi, 1968.

Hicho ni kipigo cha kwanza kwa Simba msimu huu katika Ligi Kuu Bara, pia ni cha kwanza tangu ilipochapwa kwa mara ya mwisho na Azam katika mechi ya ligi iliyopigwa Oktoba 27, mwaka jana, pia kikiwa cha kwanza kwa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye kibarua chake kimefikia tamati kuionoa timu hiyo leo.

Katika mchezo huo wa mwisho kwa Simba mbele ya Azam ilicharazwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mzambabwe Prince Dube katika dakika ya 35 na tangu hapo Wekundu hao walikuwa wakigawa dozi au kupata sare dhidi ya wapinzani waliokutana nao, ikiwamo Yanga ambao juzi walifanya kweli kwa kuikandika Simba mabao 5-1 mabao yote ya Yanga yakifungwa na nyota wa kigeni.

Kennedy Musonda aliitanguliza Yanga mapema dakika ya tatu kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba dakika ya tisa, mabao yaliyodumu hadi mapumziko na kipindi cha pili kilipoanza Yanga iliongeza mabao kupitia kwa Maxi Nzengeli aliyefunga mawili dakika za 64 na 77. Stephane Aziz Ki alifunga bao la nne na lililokuwa la saba kwake kwa msimu huu katika ligi hiyo dakika ya 73, kisha Pacome Zouzoua alihitimisha kwa mkwaju wa penalti dakika ya 87 na kuirejesha Yanga kileleni mwa msimamo ikiishusha Azam iliyokuwa imeikalia kiti baada ya kuifumua Ihefu FC kwa mabao 3-1.

Yanga imefikisha pointi 21 na mabao 25 kutokana na michezo tisa iliyocheza, moja zaidi na ile iliyocheza Simba iliyosalia na pointi 18 na mabao 17 ya kufunga na kufungwa 10 katika mechi saba ilizocheza ikiwa na kiporo kimoja dhidi ya Mashujaa ya Kigoma.

Kipigo hicho cha juzi, kilihitimisha ubabe wa Simba wa kutumia siku 373, ikiwa ni sawa na mwaka mmoja na siku tisa za kucheza mechi 28 mfululizo bila kupoteza, ikivuna jumla ya pointi 74, ikishinda mechi 23 na kudroo tano, huku ikifunga mabao 76 na kuruhusu 17 nyavuni mwa lango lao.

Katika mechi hizo 28 ambazo Simba ilicheza mfululizo bila kupoteza, 22 ni za msimu uliopita ambapo ilikusanya jumla ya pointi 56, zilizotokana na ushindi wa michezo 17 na sare tano, ikifunga pia mabao 60 na kufungwa 12, huku mechi sita zikiwa za msimu huu ambazo ilikusanya pointi 18.

Katika msimu huu kabla ya Yanga juzi kuitubulia, Simba ilikuwa imecheza mechi sita mfululizo ikishinda zote ikifunga mabao 16 na kufungwa matano tu, huku kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza akiwa kinara wa kufunga jumla ya mabao 15 akiwaongoza nyota wenzake 14 waliochangia jumla ya mabao hayo 76, likiwamo moja la kujifunga la wapinzani wao lililoibeba Simba.

Straika Mkongomani, Jean Baleke ndiye anayefuata kwa kufunga mabao mengi katika mechi hizo 28 za unbeaten ya Simba akitupia kambani mara 14, huku nahodha John Bocco akifuatia akiwa na mabao 10, ilihali nyota wa zamani wa timu hiyo aliyepo Ufaransa kwa sasa Pape Ousmane Sakho akiwa na tisa.

Mzambia Moses Phiri ndiye anayefuatia kwenye orodha hiyo akifunga mabao saba akifuatiwa na kiungo Clatous Chama aliyetupia kambani mabao matano, huku beki Henock Inonga akiwa na matatu wakati Kibu Dennis, Mzamiru Yassin, Augustine Okrah aliyerejea kwao Ghana pamoja na beki Shomary Kapombe wanafuata kila mmoja akiwa amefunga mabao mawili.

Waliofunga bao moja moja ni Israel Mwenda, Israel Mwenda, Peter Banda, Willy Onana na Fabrice Ngoma, huku Abdallah Kheri wa Azam akijifunga kwenye mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1.

Hapa kulia ni rekodi ya mechi zote 28 ambazo Simba ilicheza bila kupoteza kabla ya Yanga kuwatibulia kwa kipigo cha mabao 5-1.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live