Hafiz Konkoni, bado hajaondoka nchini, akisikilizia kwanza ishu zake kabla ya kusepa kwenda Cyprus kujiunga na timu ya Dogan Turk Birligi kwa mkopo hadi mwisho mwa msimu huu akitokea Yanga.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo Mghama amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na kufunguka mengi juu ya siku 180 alizokaa Yanga tangu aliposajiliwa kutoka Bechem United, kabla ya kutolewa kwa mkopo saa chache kabla ya dirisha dogo kufungwa Januari 15 mwaka huu.
Julai, mwaka jana, Yanga ilimtambulisha na ulikuwa ni moja ya usajili uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo hasa baada ya kuondoka kwa nyota wao, Fiston Mayele aliyekuwa mfungaji wao mahiri na alimaliza msimu wa Ligi Kuu Bara 2022/23 akiwa mfungaji bora na mabao 17.
Ujio wa Konkoni ulipokewa kwa hisia tofauti, wengi wakijiuliza kama ataweza kuvaa viatu vya Mayele.
Hata hivyo, tofauti na ilivyotarajiwa, Konkoni hakuweza kuvaa viatu hivyo na amecheza mechi nne tu na kufunga bao moja.
Dirisha la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu, lilishuhudia nyota huyu akiwa mmoja wa waliotolewa kwa mkopo na hivyo hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachomaliza msimu.
Ameenda kwa mkopo klabu ya Dogan Turk Birligi ya Cyprus hadi mwisho wa msimu.
ASHINDWA KUWA MAYELE
Kama ilivyokuwa matarajio ya wengi, angekuwa mrithi sahihi wa Mayele ambaye ametimkia Pyramid ya Misri. Hata hivyo, hakuwa akipata namba kwenye kikosi cha Kocha Miguel Gamondi na mwenyewe anasema hilo halijamwathiri chochote kwani alikuja kama Konkoni na si Mayele. Anasema hakupata muda wa kutosha wa kucheza na huenda angefanya vizuri.
Anaamini kila mtu amejaliwa na Mungu kutokana na kipaji chake. Muda unaweza ukawa sio wako akapewa mwingin, hivyo hakuna budi kukubaliana na hali.
“Kama ningepewa muda zaidi kama wengine, naamini ningefanya vizuri kama wao,” anasema Konkoni anayewatazama Didier Drogba na Zlatan Ibrahimovich kama mfano kwake.
Anasema ni kweli Yanga ina washambuliaji bora, akiwataja Clement Mzize na Kennedy Musonda. Hata hivyo, sio kwamba yeye hakuwa bora ila kutokupewa muda mrefu wa kucheza na kulimfanya aonekane sio bora.
Anaamini mchezaji yeyote anapopewa muda na kuaminiwa huongeza kujiamini na kucheza vizuri.
NI BAHATI KUCHEZA YANGA, NI KUBWA
Anasema hakuwahi kuwaza kama siku moja angekuja kucheza Yanga na alikuwa akifuatilia Ligi ya Tanzania hasa mchezo wa Dabi ya Kariakoo na huvutiwa sana na mashabiki wanavyojaa uwanjani kuutazama mchezo huo.
“Sikuwahi kuwaza kama nitakuja Yanga. Nimekuwa nikifuatilia Ligi ya Tanzania na napenda kutazama Dabi ya Kariakoo. Mashabiki wana mzuka sana na huwa wanajaza uwanja. Inavutia sana.”
“Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kule kwetu kila mtu alikuwa akifuatilia na kutaka kuifahamu na inakotoka.
“Kucheza Yanga licha ya kutokupata nafasi mara kwa mara, anaona ni bahati katika maisha yake ya soka.”
Anaongeza hata wakati ajenti wake anameeleza kuhusu Yanga alikuwa Dubai akifanya mazungumzo na Al Hilal ya Sudan, alizungumza na Idrisu Abdulah kipa wa Azam FC waliowahi kucheza timu moja na walitumia chumba kimoja wakiwa Bechem ya Ghana.
“Alinipa ABC kuhusu ligi ya Tanzania na nilirudi haraka Ghana na kusaini mkataba kwani nilivutiwa nayo. Kucheza timu iliyofika fainali kombe la shirikisho ni bahati.”
ALIITAMANI TANZANIA
Anasema ameishi maisha mazuri akiwa Tanzania na alikuwa akitamani tangu akisoma na walifundishwa kuhusu nchi hii.
“Yalikuwa maisha mazuri sana kwani nilikuwa nikiyaota muda mrefu bila kujua ni lini ndoto yangu ya kufika Tanzania itatimia licha ya panda shuka nilizopitia.
“Nikiwa shule nilisoma kuhusu Tanzania na Kisiwa cha Zanzibar na nilitamani kufika siku moja. Nashukuru kucheza Yanga imesaidia kufika na Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi japo sikukaa muda mrefu ila nilipendezwa na mandhari na watu wake ni wakarimu.”
DABI YA KARIAKOO YAMLIZA
Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza mchezo wa dabi. Sio tu Tanzania Dabi ya Kariakoo. Hata Ulaya, dabi za Manchester, El Classico na nyingine zinavutia wachezaji wengiu kujiunga na timu hizo.
Konkoni anafichua kama kuna jambo lilimkosesha raha na kufikia kulia, ni kukosa Dabi ya Kariakoo.
“Kitu kinachoniumiza zaidi ni kutokucheza Kariakoo dabi, kwani huwa ni mchezo wa tofauti na mingine kuanzia kwa mashabiki hadi kwa wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti. Nilitamani kucheza lakini nilikosa nafasi,” anasema kwa masikitiko na kuongeza.
“Siku hiyo nitaikumbuka sana, ilikuwa ni mchanganyiko wa furaha na huzuni. Baada ya kikosi kutoka sikuwa katika idadi ya wale wachezaji 21, niliumia sana niliingia ndani nikalia kwani sikufikia matamanio yangu, sikwenda hata uwanjani, lakini waliopewa nafasi walifanya vizuri, tulifunga mabao matano, nilifurahi timu kushinda, niliumia sikucheza, sikuwa na namna ni maamuzi ya kocha.”
ANA DENI KUBWA YANGA
Anasema hajafikia malengo yake Yanga na hilo ni deni kubwa kwani hajawafurahisha mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kuja kuwapa raha.
“Sio muda sahihi kuondoka Yanga. Sijafanikiwa katika malengo yangu niliyojiwekea. Bado nina deni kubwa kwani sikuwafurahisha mashabiki wa Yanga lakini sina budi kuondoka. Nashukuru kwa muda wote niliokuwa Yanga na nitaendelea kuiweka moyoni. Sina maamuzi ya kuendelea kubaki ‘Decisions are beyond my control’,” anasema.
GAMONDI MTU KWELI
Anasema Gamondi ni kocha mzuri na ingawa hakuwa anapata namba, alizungumza naye vizuri. Pia anasema waliagana vizuri na anafurahi huku akiongeza anamtakia mema pamoja na kikosi chake wafike mbali kwenye mashindano ya CAF na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
“Ni kocha mzuri sana, hata wakati naondoka nilienda kumuaga, tumezungumza mengi kuhusu soka, nina furaha kwa tuliyoyazungumza, pia nimtakie kila la kheri kwenye mashindano ya CAF na ligi kuu waweze kuchukua ubingwa.”
MORRISON KAIPAISHA BONGO GHANA
Nani asiyejua vituko vya Bernad Morrison wakati akiwa nchini. Amecheza timu zote kubwa Yanga na Simba kwa vipindi tofauti na kote alikuwa akitredi kutokana na vituko vyake hasa ishu ya usajili na staili yake ya kushangilia.
“Wakati Morisson amejiunga na Yanga alikuwa na staili yake ya ushangiliaji na kitendo hicho kilitrendi hadi nyumbani Ghana kupitia mitandao ya kijamii. Hii ilisababisha wengi kumfuatilia na hata alipohamia Simba na kurudi Yanga vyombo vya habari vilikuwa vinamfuatilia na kuzungumza kuhusu yeye.”
YANGA YAMZUIA AFCON
Anasema kukosa nafasi kwenye kikosi cha Yanga ndio kulimkatisha ndoto zake za kucheza Afcon 2023.
“Sio mara yangu ya kwanza kucheza kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana.
“Niliitwa lakini baadae niliondolewa, nilizungumza na kocha wa timu ya taifa siku moja kabla ya kutoa majina ya mwisho na aliniambia sababu kubwa ya kukatwa ni kutokuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga, kukosa muda wa kucheza na nilichukulia sawa lakini naamini nitarudi tena wakati mwingine kuitumikia timu yangu ya Taifa.”
BLACK STARS ITARUDI
Anasema kwa sasa ni kweli timu ya Taifa ya Ghana haifanyi vizuri kwenye Fainali za Afcon 2023 zinazoendelea Ivory Coast.
“Miaka ya nyuma ilikuwa inafanya vyema tofauti na sasa. Tumeanza vibaya fainali hizi na tumepoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde na kusare na Misri, ni sehemu tu ya soka kwani anaamini kuna wakati itakuwa bora kama zamani.”
ATAMMISI SKUDU/OKRAH MTAMPENDA
Anasema atawakumbuka wote wa Yanga na hasa Skudu makudubela kwani alikuwa ni Rafiki yake sana kuanzia nyumbani hadi kambini.
“Nitawamisi wote ila Skudu zaidi. Tulikuwa tunakaa chumba kimoja kambini na nyumba moja. Pia mazoezini tulienda na kurudi pamoja.”
Kuhusu Agostin Okrah, anasema anawaahidi mashabiki atafanya vizuri na watafurahi.
MASHABIKI SIKIENI
Anasema japo anajua hakuweza kuwafurahisha kama walivyotarajia lakini kwa mtu anayejua mpira hatakiwi kumlaumu sana kama wanavyofanya kwenye mitandao.
Licha ya hayo anawapenda sana na ataendelea kuwaweka kwenye moyo wake lakini anawaahidi atarudi tena.
“Najua tunatofauti zetu, lakini kikubwa nawapenda sana, walinikaribisha vizuri, kilichotekea ni sehemu ya soka, nawatakia kila la kheri, waendelee kusapoti timu lakini nitarudi tena.”
SOKA NA UALIMU
Anasema soka analipenda na ualimu pia ni kazi yake. Hata hivyo aliamua kucheza kwanza soka kwani mshika mawili moja humponyoka.
Alikuwa mwalimu wa sekondari huku akicheza kabla ya kuamua kuhamia kabisa kwenye soka na akimalizana na soka atarudi kushika chaki.
“Mimi ni mwalimu wa shule za sekondari, nilimaliza chuo nikisomea masuala ya ualimu na nilianza kufundisha huku nikicheza soka. Soka lilinipenda zaidi, hivyo, kwa sasa sifundishi lakini nikiachana na soka nitarudi kufundisha.”
Ameongeza wanasoka wasilewe na sifa za kuwa mwanasoka tu wawekeze kwenye masula mengine kutengeneza kesho yao iliyo bora, kwani maisha ya soka ni mafupi sana, lolote linaweza kutokea wakati wowote.