Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 17 za moto Simba

Simba Yaapa Kuwachapa Power Dynamos.jpeg Siku 17 za moto Simba

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Achana na suala la Simba kutinga hatua ya makundi kwa sababu sio jambo la kwanza kwao bali timu hiyo ina siku 17 za moto kutoka sasa kwa ajili ya kuwa kwenye ubora wa hali ya juu ili kutengeneza rekodi nyingine katika Ligi mpya ya Afrika (African Football League).

Simba inatarajia kucheza mechi yao ya kwanza ya African Football League, Oktoba 20, dhidi ya Al Ahly mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

Siku 17 ni katika kuandaa wachezaji kuwa fiti kila idara kuanzia, saikolojia, fitnesi, mbinu za uwanjani ili kuweza kufanya vizuri katika African Football League inayotarajia kuanza Oktoba 20 baada ya timu yao kuonekana kuwa haina makali kwa siku za hivi karibuni.

Kabla ya kuanza kwa Ligi hiyo, Simba itakuwa na mechi mbili za Ligi Kuu zote ikiwa ugenini dhidi Tanzania Prisons (Oktoba 5) na Singida Big Stars (Oktoba 8) ambazo zitawafanya warekebishe makosa ambayo timu hiyo imeonyesha katika mechi zao.

Mashabiki wa Simba ambao wamekuwa wakijitokeza uwanjani hawakubaliani na kile kinachoonekana na hata wale wa mitandaoni maneno yao katika mitandao ni wazi kabisa hawafurahishwi na namna ambavyo timu hiyo inacheza kwa sasa licha ya kwamba haijafungwa mechi yoyote ile lakini haionyeshi makali yake.

Katika mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa, wachezaji wa Simba wamekuwa wakicheza kama vile wamechoka hali ambayo wadau mbalimbali wanakiri inawezekana kabisa upande wa fitinesi ni ndogo kwa mastaa wao.

Wakati huohuo, bao ambalo Simba iliruhusu katika mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos uliomalizika kwa sare 1-1 limeonyesha mapungufu mengine ya wachezaji wake kutokaba.

Bao hilo lililofungwa na Andy Boyeli alifunga akiwa amezungukwa na wachezaji nane wa Simba ambao ni Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone, Kennedy Juma, Kibu Denis na Fabrice Ngoma.

Bao hilo ni sawa na lile ambalo walifungwa wiki mbili zilizopita (bao la pili) katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Power Dynamos lililofungwa na Mulombwa ambaye alifyatuka shuti nje ya boksi akizungukwa na wachezaji sita wa Simba, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Shomari Kapombe, Henock Inonga, Mohamed Hussein na Che Malone.

Wachezaji wa Simba kwa nyakati tofauti hoja zao zimeungana zikihitaji mastaa wa timu hiyo waache umwinyi na badala yake waipambanie jezi katika kumwaga jasho.

Mshambuliaji wa zamani Simba, Emmanuel Gabriel alisema timu hiyo haina tatizo kubwa badala yake ni wachezaji hawajitoi katika dakika 90 kuitumikia timu yao.

"Wakae na wachezaji na kuwaambia waache umwinyi, Simba ukiangalia ni hawazidi wachezaji wanne ambao wanamwaga jasho;

"Hakuna kusema kipa wala kocha kwa sababu wachezaji hawajitumi ndani ya uwanja, kocha kwani si ndio huyo msimu uliopita alikuwepo."

Upande wa Bakari Kigodeko alisema wachezaji wanatakiwa wajitume na wakiwa katika levo sawa basi itakuwa rahisi kupatikana kwa kikosi cha kwanza.

"Simba hadi sasa haina muunganiko mzuri, hakuna kikosi cha kwanza chenye uhakika ndani ya uwanja;

"Huku kwenye Ligi hiyo unayosema siku 17 ni chache na ukisema utumie nguvu basi wachezaji wataumia lakini wanaweza kurekebisha makosa kwa kuanzia ngazi ya beki na kiungo, viungo wakabaji na wachezeshaji waongeze nguvu kwenye majukumu yao."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live