Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 10 zimetimia, licha ya mabango, mapumziko yanatumikaje?

Simba Vs Yanga Aziz Ki Debut.jpeg Siku 10 zimetimia, licha ya mabango, mapumziko yanatumikaje?

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Leo Jumatano zimetimia siku 10 tangu wadau wa soka Tanzania na wapenzi wa timu za Simba na Yanga kupata mshtuko, kufuatia mashindano ya kushangaza ya dabi ya Kariakoo ambapo mchezo huo ulishuhudiwa ukimalizika kwa Simba kupokea kipigo cha mabao 5-1.

Nimesema yalikuwa matokeo ya kushtusha hasa kwa kuwa mchezo huu kwa kawaida unakuwa na upinzani mkubwa wa ndani na nje ya uwanja, hivyo ni vigumu kwa timu kuruhusu kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.

Ikumbukwe mara ya mwisho kushuhudia matokeo kama hayo ni zaidi ya miaka 12 iliyopita ambapo wakati huo ni Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga.

Tangu kipigo hicho cha Simba, tumeshuhudia matukio mengi ya kufurahisha ya kudumisha utani ambapo Yanga wanaendelea kufurahia ushindi huo, ambapo walianza na ‘SUPU DAY’ iliyofanyika siku ya Jumapili ambapo wadau mbalimbali wa timu hiyo walikutana pamoja na kunywa supu na chapati kama sehemu ya kukumbuka ushindi wao. Kama hiyo haitoshi Yanga jana Jumanne asubuhi wakaamka na mabango ya barabarani ya matokeo ya mchezo wao na Simba. Kwa mashabiki wa Simba hii kero ya watani zao ni muhimu wakaichukulia kwa upande chanya kwa kuhakikisha watendaji wao wanashughulikia changamoto zinazowakabili kwa ufasaha na mashabiki watimize jukumu lao la kuwasapoti wachezaji na viongozi wao.

Hayo yote yametokea wakati ligi ikiwa imeingia katika mzunguko wa nane na mabingwa watetezi Yanga wao wanaongoza msimamo wa ligi na pointi zao 21. Baada ya mizunguko hiyo nane, ligi kwa sasa ipo kwenye mapumziko ya muda kupisha mashindano ya kimataifa ya michezo ya timu za Taifa.

Ni wazi kuwa ligi ya msimu huu imeonekana kuwa na ubora mkubwa kulinganisha na zile za misimu iliyopita, hali ambayo inatajwa kuchagizwa zaidi na mazingira ya kuboreshwa kwa maslahi ya klabu kupitia mikataba minono ya udhamini ambayo Shirikisho la soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeingia na makampuni mbalimbali yanayohitaji kujitangaza kibiashara.

Muda huu wa mapumziko ambayo inawezekana si rasmi sana unapaswa kuwa na faida kwa timu zote shiriki ambazo zinapaswa kuhakikisha zinajiandaa vizuri kwa ajili ya michezo yao ijayo mara baada ya ligi kurejea.

Hivyo muda huu wa mapumziko ni wakati muhimu kwa timu kujiandaa vizuri, ili pale watakaporejea wawe na utimamu wa kutosha wa miili kwa ajili ya kupambana hususani kwa timu ambazo zina mashindano mengine ya kimataifa.

Baada ya mizunguko hiyo nane ya kwanza kukamilika, tumeshuhudia wachezaji wengi wakipata majeraha ya mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugumu wa ligi na changamoto za muda wa maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’, hivyo huu kwao ni muda sahihi kutengeneza hiyo ‘fitness’ na kuwa na msaada kwenye vikosi vyao.

Ni matumaini yangu kuona namba ya majeruhi wakipungua baada ya kumalizika kwa kipindi hiki kwa kuwa wachezaji wengi watapata nafasi ya kupumzika vya kutosha na kufanya mazoezi ya kuwaongezea utimamu wa miili yao.

Tukumbuke msemo wa waswahili usemao: “Biashara asubuhi, jioni mahesabu.” Hivyo kila mtu achange karata zake vizuri mapema kabla ya mambo hayajabadilika na kuwa magumu mwishoni.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live