Bado siku 10 zitakazoamua nani atakuwa bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) huku ushindani ukiwa kwa timu tatu, JKT Queens, Simba Queens na Fountain Gate Princess. Msimu uliopita Simba Queens walichukua ubingwa huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Fountian Gate Princess.
JKT Queens inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 40 akifuatiwa na Simba Queens yenye pointi 39 huku Fountain Gate ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38. Kila timu hadi sasa imecheza michezo 16 ikibakiza michezo miwili kumaliza ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Mei 17 mwaka huu.
Kazi itakuwepo katika mchezo unaofuata utakaochezwa Mei 10 katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa kati ya Fountain Gate Princess na JKT Queens ambao unaweza ukaamua nani anakuwa bingwa.
Simba imebakiza michezo dhidi ya Baobab Queens (Mei 10) utachezwa Uwanja wa Jamhuri na Mei 17 itamaliza kazi dhidi ya Ceasiaa Queens ya mkoani Iringa katika Uwanja wa Chuo cha Mkwawa Iringa.
JKT imebakisha dhidi ya Fountain Mei 10 mwaka huu itakayochezwa Uwanja wa Jamhuri na itamaliza dhidi ya Mkwawa Queens mkoani Iringa, Mei 17 mwaka huu.
Fountain ina mechi na JKT Queens (Mei 10) itamaliza Mei 17 dhidi ya The Tiger katika Uwanja wa Jamhuri.
Kocha wa Fountain Gate, Juma Masoud alisema baada ya ushindi dhidi ya Ceasiaa Queens wanajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri michezo yao miwili ya nyumbani dhidi ya JKT na The Tiger.
Huku kocha wa JKT Queens, Ally Ally akisema wamekula ng’ombe kilichobaki ni kumalizia mkia lakini watacheza kwa tahadhari michezo iliyobaki ikiwemo ule na Fountain Gate Princess.